Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
QURAN

Surat Yunus 5-10

2016/01/19

Surat Yunus 5-10

Surat Yunus 5-10

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.

Sura ya10 inayoitwa Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na tunaianza kwa aya ya 5 na 6 za sura hiyo ambazo zinasema:

"Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye aliyelifanya jua kuwa mwanga, na mwezi kuwa nuru na akaupimia vituo(huo mwezi) ili mujue idadi ya miaka na hisabu (nyinginezo). Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa haki. Anazipambanua ishara (zake) kwa watu wanaotaka kujua."  "Hakika katika mfuatano (wa daima) wa usiku na mchana ; na katika alivyoviumba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi ziko ishara kwa watu wanaomcha Mungu."

Baada ya aya za mwanzoni mwa sura hii kuashiria juu ya kufufuliwa, kama tulivyoona katika darsa iliyopita, aya hizi tulizosoma zinagusia sehemu ndogo tu ya madhihirisho ya adhama ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji kwa kuzungumzia nafasi ya jua na mwezi. Uhai wa wanaadamu na sayari yenyewe ya dunia vinategemea nuru na joto litokanalo na jua kama ambavyo nuru ya kupendeza ipatikanayo kupitia kwenye mwezi huwa mithili ya mwanga wa kulalia kwa viumbe mbali mbali wakiwemo wanadamu na pia hutumiwa kama kurunzi ya kuongozea njia katika safari za majangwani na baharini za viumbe hao. Lakini pia kama tunavyojua mwendo wa sayari ya dunia wa kulizunguka jua na ule wa mwezi wa kuizunguka dunia ndivyo vinavyotuwezesha kuwa na hesabu za siku na pia mwaka kulingana na kalenda ya jua yaani shamsia. Aidha kutokana na mabadiliko ya umbo la mwezi kuanzia hilali hadi mwezi kamili, ndivyo tunavyoweza kupata pia hesabu ya miezi 12 kulingana na kalenda ya Hijria. Aya zinamalizia kwa kutilia mkazo nukta hii kwamba yote hayo yaani mfumo kamili wa uumbaji vimefanywa kwa ajili ya kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu ni wa haki na yote hayo ameyafanya kwa hikma kubwa na kwamba mabadiliko tunayoshuhudia kila siku ya kubadilika kwa usiku na mchana ambayo wengi wetu tunayachukulia kuwa ni kitu cha kawaida, ni dhihirisho la uwezo na hikma ya Allah sw ambalo wanalidiriki na kulihisi wale wamchao yeye Mola Mwenyezi. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa idadi, hesabu na tarakimu ni vitu vyenye umuhimu katika maisha ya mwanadamu, na quran inatuonyesha kuwa kuhesabu masiku ya mwezi na mwaka kwa kutumia jua na mwezi ni miongoni mwa njia za kutumia kwa ajili ya kufanyia hesabu hizo. Funzo jengine na ambalo ni la kuzingatiwa sana katika aya hizi ni kuwa haifai kwa muislamu kuvipita vivi hivi vitu vya kimaumbile vilivyomzunguka, kwani katika vitu hivyo anaweza kushuhudia kwa karibu adhama yake Mola Muumba.

Zifuatazo sasa ni aya za 7 na 8 ambazo zinasema:

"Hakika wale wasiotaraji kukutana nasi na wakaridhia maisha ya dunia na wakatua kwa hayo, na walioghafilika na ishara zetu." "Hao makaazi yao ni motoni kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma."

Baada ya aya zilizotangulia kubainisha ishara za kuwepo Allah sw kupitia uumbaji wa mbingu na ardhi aya hizi zinasema wale walioghafilika na ishara hizo na kushindwa kuzidiriki ishara za kuwepo Mwenyezi Mungu, uwezo wake na hikma yake huishia katika kuikumbatia dunia ya kupita wakidhani kuwa kila kitu kinaishia hapa.Hivyo huwa hawafikirii juu ya kukutana na Mola wao siku ya Kiyama, na ndiyo maana mwisho wa watu hao unakuwa ni kwenda kutumbukizwa kwenye moto wa jahannam huko akhera.

Moja kati ya mafunzo muhimu tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa kughafilika na Kiyama na kuipaparikia dunia ndiyo mambo yanayomfanya mtu atumbukie kwenye ufuska na maasi.

Darsa yetu tunaihitimisha kwa aya za 9 na 10 ambazo zinasema:

"Hakika wale walioamini na wakatenda mema Mola wao Mlezi atawaongoa kwa sababu ya imani yao. Itakuwa inapita mito mbele yao katika mabustani yenye neema." "Wito wao humo utakuwa: Subhanakallahumma! Umetakasika Ee Mwenyezi Mungu. Na maamkiano yao humo ni salamun (Alaykum). Na wito wao wa mwisho ni :Alhamdulillahi Rabbil Aalamin"Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu. Mola Mlezi wa walimwengu wote."

Wakati aya zilizotangulia zimebainisha hali ya adhabu itakayowapata wale walioamua kuiabudu dunia, aya hizi zinaashiria hali ya waumini watakaoingizwa peponi na kusema kuwa kupata uongofu wa Allah ndiyo hazina kubwa waliyokuwa nayo watu hao tabaan waliipata kutokana na kumwamini Mola wao na kufanya amali njema. Kisha aya zinaashiria dua na dhikri za watu wa peponi na kusema kuwa utajo wa Subhanallah na Alhamdulillah ni miongoni mwa alama za watu hao, lakini kama tujuavyo dhikri hizo haziishii katika kuzitamka kwa ulimi tu bali mtu anatakiwa awe anaitakidi kwa dhati kuwa Allah sw ametakasika na kila kasoro na upungufu, na ni kwa kufahamu hivyo ndipo mja humhimidi na kumshukuru kwa dhati Mola Mwenyezi kwa sifa zake zote za ukamilifu. Aya hizi wapenzi wasomaji zinatuoyesha kuwa uongofu wa Allah ni kitu anachokihitajia katika lahadha ya uhai wake. Aidha aya zinatuonyesha kuwa maamkizi ya amani, ndiyo yatakayotawala katika anga ya peponi. Maamkizi ya amani yatakayotoka kwa Mwenyezi Mungu, yatakayotoka kwa Malaika, na pia watakayopeana watu wa peponi wao kwa wao. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa watu hao. Amin.