Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
QURAN

Surat Yunus 19-23

2016/01/19

Surat Yunus 19-23

Surat Yunus 19-23

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Assalaamu Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'an. Hii ni darsa ya 310, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya ya 19 ambayo inasema:

"Wala watu hawakuwa ila umma mmoja tu. Kisha wakakhitalifiana. Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka hukumu ingelikwisha katwa baina yao katika hayo wanayo khitalifiana."

Mwenyezi Mungu sw amewaumba wanaadamu wote wakiwa na fitra yaani maumbile safi ya tauhidi ya kukubali kuwepo kwa Mungu mmoja. Hivyo hapo awali wanaadamu wote walikuwa ni sawa na umma mmoja. Lakini kwa kupita muda, na kuzainiwa na shetani kundi miongoni mwa watu wakatumbukia kwenye upotofu wa shirki na hivyo watu wakagawika katika makundi mawili; ya wampwekeshao Allah na Mushrikina. Ama Mwenyezi Mungu hakutaka kuwateza nguvu waja wake, bali alitaka kila mtu achague kwa hiyari yake njia anayoamua kufuata. Na ni kwa sababu hiyo ndipo akaamua kuwapa fursa na muhula wale waliokhitari upotofu kufanya lolote lile watakalo. Na lau si utaratibu huo aliouweka Mwenyezi Mungu basi angewaadhibu papa hapa duniani na kumaliza hitilafu kati ya waumini na makafiri. Funzo mojawapo tunalopata katika aya hii ni kuwa thamani na utukufu wa mwanadamu unapatikana kwa kule kufanya ayatakayo ikiwa ya thawabu au ya madhambi kwa hiyari yake. Vinginevyo hakuna fakhari yoyote kwa mtu kuamini na kufuata njia ya haki kwa kulazimishwa.

Ifuatayo sasa ni aya ya 20 ambayo inasema:

"Na wanasema: Kwa nini hakuteremshiwa kutoka kwa Mola wake miujiza (tunayoitaka)? Sema: Mambo ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu.Basi nyinyi ngojeni, na mimi ni pamoja na nanyi katika wanaongoja."

Nabii Muhammad (s) alikuja na miujiza mbali mbali kama walivyokuwa Manabii waliomtangulia. Tabaan muujiza mkuu wa Mtume huyo wa mwisho ni Quran tukufu ambayo washirikina walishindwa kukabiliana nayo hata kwa kuleta walau aya moja mfano wake. Lakini katika kutafuta visingizio, washirikina hao kila siku walikuwa wakitaka waonyeshwe muujiza mpya ikiwa ni pamoja na kumtaka Bwana Mtume (s) awaletee kila wanachotaka. Ndipo katika kuwajibu Bwana Mtume (s) akawaambia muujiza ni suala lililoko kwenye mamlaka ya Mwenyezi Mungu na wala haliko mikononi mwangu mimi, na ni kila pale anapotaka yeye ndipo muujiza unapoletwa, ama mnachotaka nyinyi si kitu kingine ghairi ya kutafuta visingizio tu. Ukweli wa haya wapenzi wasomaji unashuhudiwa pia kama tulivyoona katika aya zilizotangulia pale washirikina wa kikureishi walipomtaka Bwana Mtume (s) azibadilishe aya za quran au hata ikiwezekana awaletee qurani nyingine mpya badala ya ile aliyoteremshiwa na Mola wake. Pamoja na mambo mengine aya hii inatufunza kuwa chanzo na chimbuko la shirki na ukafiri si kutokuwepo muujiza na hoja za kuthibitisha ukweli wa risala ya haki, isipokuwa ni tabia ya ukaidi, inda na inadi mbele ya haki. 

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 21 ambayo inasema:

"Na tunapowaonjesha watu rehma baada ya shida iliyowapata, mara huanza kutunga hila (za kutaka kupinga) Aya zetu. Sema: Mwenyezi Mungu ni mwepesi zaidi wa kupanga. Hakika wajumbe wetu wanayaandika mnayoyapanga."

Historia inasimulia kuwa ilitokea wakati mmoja mji wa Makka ulikumbwa na ukame mkubwa lakini Mwenyezi Mungu kwa baraka ya kuwepo Nabii Muhammad (s) akateremsha mvua zake za rehma na kuuletea faraja mji huo. Ama washirikina wao walidai kuwa kunyesha kwa mvua hizo kulitokana na baraka za masanamu yao. Ndipo aya tuliyoisoma ikashuka na kuwatanabahisha kuwa kama nyinyi ni wenye kutaka hakika ya mambo, basi tambueni kuwa mvua hiyo ilikuwa ni muujiza utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo inadi yenu imekufanyeni muzue hila hizi na zile za kuzinasibisha na masanamu yenu rehma hiyo iliyotoka kwa Mola wenu. Pamoja na hayo tambueni kuwa malaika wa Mwenyezi Mungu ambao hutumwa kwa watu wanayanakili na kuyarekodi yote yanayotendwa na waja na hivyo mushirikina wajiandae na majibu ya kwenda kumpa Mola wao siku ya kiyama kwa yote wanayoyatenda. Tabaan katika dunia hii pia Mwenyezi Mungu atawapa jaza ya vitimbi na hila zao, nao katu hawawezi kusimama dhidi ya irada ya Allah SW. 

Aya za 22 na 23 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

"Yeye ndiye anayekuendsheni bara na baharini. Hata mnapokuwa majahazini na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia, mara upepo mkali ukawazukia na yakawajia mawimbi kutoka kila upande na wakaona wameshatingwa, hapo ndipo wanapomwomba Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia utii (wakisema): Ukituokoa na haya bila shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru." "Lakini akishawaokoa mara wanafanya jeuri tena katika ardhi bila ya haki.Enyi watu! Jeuri zenu zitakudhuruni wenyewe. Ni starehe (chache tu) za maisha ya dunia. Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo tutakuambieni mliyokuwa mkiyatenda."

Bila shaka mngali mnakumbuka wapenzi wasomaji kuwa tulisema mwanzoni mwa darsa yetu hii kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba wanaadamu wote katika fitra na maumbile safi ya tauhidi ya laa ilaha illa llah, yaani kukana waungu wengine wote bandia na kuthibitisha hakika ya kuwepo kwa Mola mmoja tu wa haki. Baada ya kueleza hayo, aya hizi tulizosoma hivi punde zinabainisha kuwa mapumbao haya na yale ya kidunia huwa mithili ya utando unaogubika na kufililiza nuru hiyo ya tauhidi ndani ya nafsi ya mtu na kumfanya mja aghafilike na Mola wake. Ama pale mtu anapotingwa na kupatwa masaibu yanayomfanya akate tamaa ya kupata nusra kupitia njia yoyote ile, hapo ndipo utando ule unapotoweka mithili ya vumbi lililosukumwa na upepo na kuiamsha fitra na maumbile ya tauhidi, na kumshuhudia mja akimlingana na kumwomba kwa ikhlasi na unyenyekevu Mola wake aliyemuumba msaada wa nusra na uokozi. Lakini kama tulivyowahi kuashiria katika moja ya darsa zilizopita baada ya kupata nusra ya Allah mwanadamu husahau kila kitu mara moja, akighafilika kwamba maisha haya ya dunia ni mafupi na ya kupita tu, na kwamba sisi sote mwisho wetu na marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu, na huko kila mmoja atasimamishwa mbele ya mahakama ya uadilifu ili kuwajibika kwa yote aliyoyafanya hapa duniani. Aya hizi zinatuoenyesha kuwa majanga ya kimaumbile husaidia kuondoa ghururi na kiburi cha mwanadamu na kuamsha hisia za kumtambua na kumnyenyekea Mola wake. Aidha aya zinatutaka tuelewe kuwa imani ya msimu na ya mazingira fulani haina faida; imani ya kweli ni ya kudumu na ya katika kila hali, awe mtu katika raha na neema au shida na nakama. Darsa ya 310 inaishia hapa.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wale wanaomwamini na kuikiri tauhidi katika hali zote. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.