Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
QURAN

Surat Yunus 28-33

2016/01/19

Surat Yunus 28-33

Surat Yunus 28-33

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Assalaamu Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'an. Hii ni darsa ya 312, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya za 28 na 29 ambazo zinasema:

"Na siku tutakapowakusanya wote, kisha tutawaambia wale walioshirikisha:Simameni mahali penu nyinyi na wale mliowafanya washirika wa Mungu.' Kisha tutawatenga baina yao. Na hao waliowashirikisha watasema: Nyinyi hamkuwa mkituabudu sisi.'" "Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yetu na baina yenu. Hakika sisi tulikuwa hatuna habari ya ibada yenu."

Aya hizi zinabainisha jinsi hali itakavyokuwa siku ya Kiyama, ambapo Mwenyezi Mungu atawasimamisha mushirikina na wale waliokuwa wakiwaabudu na kuliuliza kila kundi peke yake; kwa nini nyinyi mlikuwa mkiyaabudu masanamu na miungu wa kubuni? Na nyinyi pia ilikuwaje mkaridhia kuabudiwa na watu hawa? Hapo ile miungu ya masanamu isiyo na uhai itapewa uhai kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuwakana wale waliokuwa wakiwaabudu na kutamka kuwa, "sisi hatukuwa tukijihesabu kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu, bali nyinyi mlijitengenezea taswira akilini mwenu, na kuziabudu na sisi kutufanya kama kisingizio tu".

Aya ya 41 ya suratu Sabaa pia imeashiria maudhui hii na kueleza kuwa malaika nao ambao walikuwa wakiabudiwa wanadhihirisha, kuchukizwa kwao na kitendo hicho cha Mushrikina. Nukta yenye mguso wa aina yake hapa ni kuwa katika aya hizi Allah sw amewataja waabudiwa hao kuwa ni washirika wa Mushrikina kwa maana kwamba, hao hawakuwa waungu wanaoshirikishwa na Mwenyezi Mungu, bali ni washirika wenu nyinyi mushirikina mliojibunia na kujitengenezea wenyewe. Miongoni mwa yale tunayojifunza katika aya hizi ni kuwa siku ya Kiyama, mbali ya wanaadamu, miungu na waabudiwa bandia yakiwemo masanamu yatapewa uhai ili kutoa ushahidi katika mahakama ya uadilifu dhidi ya mushirikina. 

Ifuatayo sasa ni aya ya 30 ambayo inasema:

"Huko kila mtu atayajua aliyoyatanguliza. Na watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki. Na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyazua."

Baada ya masanamu na waabudiwa wengine kuwakana mushirkina, hapo makundi mawili hayo yatatenganishwa na mushirikina hawatoweza kuwaomba msaada hao waliokuwa wakiwafanya washirika wa Mwenyezi Mungu hapa duniani, na badala yake watarejea kwa Mola wao wa haki yaani Allah sw na hapo ndipo watapata jaza na malipo ya amali zao. 

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 31 ambayo inasema:

"Sema: Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na katika ardhi. Au ni nani anayemiliki kusikia na kuona? Na ni nani amtoaye mzima katika mfu na kumtoa mfu katika mzima? Na nani anaye yadabiri mambo yote?' Watasema: €˜Ni Mwenyezi Mungu.' Basi sema: Je Hamuogopi?"

Baada ya aya zilizotangulia ambazo zimeonyesha unyonge na udhalili utakaowapata washirikina siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake awaulize watu hao kuwa nyinyi ambao mnamkubali Mwenyezi Mungu, na mnajua kuwa ni yeye ndiye anayekuruzukuni, na ni yeye ndiye anayesimamia mambo yenu yote, kwa nini basi badala ya kumwabudu yeye mnayaabudu masanamu na kuyafanya wasita na waunganishi wa mambo yenu kwa Mwenyezi Mungu? Kama ambavyo katika aya nyingine za quran imeelezwa kuwa mushirikina wa enzi za ujahiliya walikuwa wakikubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wao na Muumba wa ulimwengu, ama katika suala la kuendesha mambo, mamlaka hayo yako mikonnoni mwa malaika na vitu vingine vya maumbile, kama kwamba Mwenyezi Mungu ameumba tu kisha akakaa kando na kulikabidhi kwa viumbe hao suala la uendeshaji wa ulimwengu. Fikra ya aina hii imeelezwa na quran tukufu kuwa ni batili na aina mojawapo ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Funzo mojawapo tunalopata katika aya hii ni kuwa uendeshaji wa ulimwengu unahitajia tadbiri isiyobadilika, na hili halingewezekana kama kungekuwepo na Muumba zaidi ya mmoja. 

Aya za 32 na 33 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

"Basi huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu wa haki. Na kipo kitu gani baada ya haki isipokuwa upotofu tu? Basi huwaje mkageuzwa?" "Hivi ndivyo kauli ya Mola wako itakavyowathubutikia wale walioasi, ya kwamba hawataamini."

Baada ya aya zilizotangulia kubainisha mifano ya ishara za adhama ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa mbingu na ardhi pamoja na kukiri kwa washirikina kuhusu uumbaji wa Mwenyezi Mungu, aya hizi zinabainisha wazi kuwa Mungu huyu ndiye Mola wenu, na vile vile ndiye muendeshaji mambo yenu; na si kwamba yeye ni muumba wenu lakini masanamu yakawa ndio waendeshaji wa mambo yenu. Kisha aya zinaendelea kwa kutoa kauli ya mkato kwamba, hakuna hali ya tatu baada ya haki na batili. Kwa maana kwamba kila kitu ima ni haki au ni batili, na kwa hivyo kwa kuwa Mwenyezi azza wa jal ndiye haki, basi bila shaka masanamu na miungu wenu wengine wa kubuni hawawezi kuwa haki, na hivyo wale watu wanaoamua kuipa mgongo haki kwa inadi, ubishi na ukaidi hawawezi kupata taufiki ya kuufikia uongofu. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa hakuna njia ya tatu baada ya haki na batili. Na kwa hivyo yanapothibitika mawili hayo, hakuna nafasi ya mtu kudai kuwa yeye hayuko huku wala huku bali ni mtu wa kati na kati. Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuepushe na shirki na kuijenga imani kamili na safi ya tauhidi ndani ya nyoyo zetu. Amin

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.