Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
QURAN

Surat Yunus 24-27

2016/01/19

Surat Yunus 24-27

Surat Yunus 24-27

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, darsa hii tunaianza kwa aya ya 24 ambayo inasema:

"Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mawinguni, kisha mimea ya ardhi wanayoila watu na wanyama ikachanganyika nayo (maji hayo, ikastawi). Hata ardhi ilipokamilika uzuri wake na ikapambika, na wenyewe wakadhani wameshaiweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana na tukaifanya kama iliyofyekwa, kama kwamba haikuwako jana. Namna hivi tunazipambanua aya (zetu) kwa watu wanaofikiri."

Katika kubainisha baadhi ya masuala, Mwenyezi Mungu ametumia ndani ya quran lugha ya tamthili na tashbihi. Aya tuliyoisoma ni miongoni mwa aya hizo ambayo imelinganisha na kushabihisha hali ya kupita na kumalizika haraka dunia kuwa ni sawa na ardhi iliyonawiri kutokana na kunyeshewa na mvua lakini pale inapokuja kukumbwa na kimbunga au mafuriko tahamaki kila kitu kilichopandwa katika ardhi hiyo kinatoweka kana kwamba havikuwepo hapo kabla. Aya hii wapenzi wasomaji inatuelimisha kuwa umri wa mwanadamu katika dunia hii ni mfupi mithili ya umri wa mimea na maua hivyo tusihadaike tukadhani kuwa tutabaki milele katika ulimwengu huu. 

Ifuatayo sasa ni aya ya 25 ambayo inasema:

"Na Mwenyezi Mungu anaita kwendea nyumba ya amani, na humuongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka (maadamu anakubali uwongofu)."

Mkabala wa maisha haya ya mafupi na ya kupita ya dunia kuna maisha mengine ya milele ya akhera ambayo Mwenyezi Mungu amewataka waja wake wayapiganie hayo na akawapelekea Mitume pia wa kuongoza watu kuelekea kwenye makazi ya utulivu wa kweli . Ni wazi kuwa watu wanaoshikamana na kamba ya uongofu ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewahisi kuwa wana ustahili wa kufikia makazi hayo na ambao matendo na amali zao hapa duniani hazikuwa sababu ya kujiweka mbali na njia iliyonyooka. Aya hii, inatufunza kuwa raha na uzima wa dunia ni vitu vya kupita tu. Kinyume chake, raha na uzima wa akhera ni za kudumu na za milele. Funzo jengine tunalolipata katika aya hii, ni kuwa njia pekee ya kufikia kwenye utulivu na raha za kweli ni kupiga hatua kuelekea kwenye njia ya iliyonyooka ya Allah, ambayo hapa duniani huupa moyo wa mja utulivu na huko akhera humuongoza kuelekea kwenye pepo ya saada.

Tuitegee sikio sasa aya ya 26 ambayo inasema:

"Wale waliofanya wema watapata (jaza ya) wema (wao) na ziada; Wala vumbi halitawafunika nyuso zao wala madhila. Hao ndio watu wa Peponi; humo watakaa milele."

Baada ya aya iliyotangulia kuashiria juu ya pepo, aya hii inasema Mwenyezi Mungu ameiandaa pepo hiyo kwa wale waja wake waliofanya mema, na kwamba jaza na malipo watakayopata waja hao iwe ni kwa sura ya wingi au ubora, yatakuwa makubwa na bora zaidi kuliko amali walizotenda hapa duniani na kama ambavyo katika aya nyinginezo Allah sw anasema yeyote atendaye jema moja hupata thawabu na malipo mara kumi ya jema hilo, ambapo kwa upande wa utoaji, malipo ya mja hufikia hata mara mia saba ya kile alichokitoa. Baadhi ya yale tunayojifunza katika aya hii ni kuwa, ikiwa Mwenyezi Mungu ametuita tuifuate njia yake ya uongofu kisha akatuonyesha njia ya kuifikia, na kisha akatushajiisha na hata kuwalipa thawabu na malipo bora kabisa wale wanaoifikia njia hiyo, ni kitu gani basi cha kutufanya tuache kuitikia mwito wa Mola wetu na kuwafuata wengine wasiokuwa yeye? 

Aya inayotuhitimishia darsa yetu ni ya 27 na ambayo inasema:

  "Na wale waliochuma maovu, malipo ya uovu ni mfano wake vile vile; na yatawafika madhila. Hawatakuwa na awezaye kuwalinda na (adhabu ya) Mwenyezi Mungu. Zitakuwa nyuso zao kama kwamba zimefunikwa na vipande vya usiku wa giza. Hao ndio watu wa Motoni; humo watakaa daima."

Wakati ambapo wale waliotenda matendo mazuri watakuwa na mwisho mwema huko akhera, wale waliokhitari kufuata upotofu kwa kumkufuru na kumwasi Mola wao hawatapata jaza nyingine ghairi ya adhabu ya Allah, na wala hawatoweza, wala kupata pa kukimbilia, ambapo ukali wa adhabu watakayopata utazifanya nyuso zao zititie na kupiga weusi. Tabaan adhabu hiyo italingana kabisa na uzito na kiwango cha madhambi waliyofanya, ama kwa upande wa watenda mema wao watapata fadhila zake Mola za kulipwa malipo ya kheri yaliyo makubwa zaidi ya mema waliyotenda. Aya hii pamoja na mambo mengine inatuelimisha kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba wanaadamu akiwa amewapa uhuru na hiyari ya kuchagua njia ya kufuata. Na ndiyo maana kundi moja linaamua kufuata mema na jengine linakhitari kufuata maovu. Halikadhalika aya inatufunza kuwa katika mfumo wa malezi wa Uislamu siku zote ushajiishaji kwa kutoa hidaya na zawadi unapewa kipaumbele kuliko utiaji adabu na utoaji adhabu.

Darsa ya 311 inaishia hapa. Tunamwomba Allah ajaalie bora ya amali zetu ziwe ni zile za lahadha ya mwisho ya uhai wetu, na siku bora kwetu iwe ni ile ya kukutana na yeye.

Amin Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.