Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
QURAN

Surat Yunus 1-4

2016/01/19

Surat Yunus 1-4

Surat Yunus 1-4

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Ifuatayo ni tarjuma na maelezo mafupimafupi ya Sura ya 10 ya Qur'ani Tukufu ambayo inaitwa Surat Yunus.

Jina la sura hii linatokana na jina la Nabii Yunus as, ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu aliyekuja baada ya Manabii Nuh na Musa as.

Tunaianza basi darsa yetu hii kwa aya ya kwanza na ya pili za sura hiyo ambazo zinasema:

Alif lam Ra. Hizi ni aya za kitab chenye hikima. Je ni ajabu kwa watu ya kwamba tumemfunulia wahyi mtu miongoni mwao kuwa: "Waonye watu na wape walioamini habari njema ya kwamba watakuwa na cheo kikubwa mbele ya Mola wao?". Wakasema makafiri: "Hayakuwa haya ila ni kiini macho".

Kama tulivyowahi kueleza wakati tulipoizungumzia sura ya pili ya al Baqarah, ni kwamba kati ya sura zote 114 za quran tukufu, sura 29 kati yao zinaanza kwa herufi za mkato kama alif lam mim, hamim, yasin n.k. Na tukasema kuwa, kwa kuwa aya zinazofuatia baada ya aya hizo mara nyingi huzungumzia adhama ya quran, baadhi ya wafasiri wanasema lengo lililokusudiwa katika kutanguliza aya hizo ni kutolewa changamoto kwa wasioiamini quran, kwa maana kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha quran kwa kutumia herufi hizo, hivyo nanyi pia kama mnao uwezo teremsheni quran mfano wa hiyo. Mojawapo ya sifa ambazo Mwenyezi Mungu ameitaja kuwa kimepambika nayo kitabu chake kitukufu cha quran ni hikima. Na hii ni kwa sababu hukumu za dini zilizokuja ndani ya kitabu hicho zimesimama juu ya hoja madhubuti na yale yaliyomo ndani yake ni mafunzo yenye hekima kubwa. Baada ya kueleza hadhi na nafasi ya quran, katika aya ya pili Mwenyezi Mungu anabainisha nafasi na hadhi ya Mtume wake na kueleza kuwa watu wanatarajia kuona Mwenyezi Mungu akiteremsha Malaika kwa ajili ya kuwafikisha wao uongofu ,wakati kwa kuwa wao ni wanaadamu akili inahukumu kwamba Mtume atakayetumwa kwao lazima naye awe ni mtu kama wao, na anayezungumza lugha yao ili matendo na mwenendo wake wa maisha uweze kuwa kigezo kwao. Kazi ya Mitume hao ni kutoa bishara njema kwa wafanyao mema na kuwaonya wale watendao mabaya. Lakini kutokana na baadhi ya wakati kuonyesha miujiza ya kuthibitisha ukweli wa unabii wao, baadhi ya watu wasiokuwa tayari kuiamini haki huwasingizia Mitume hao kuwa ni wachawi. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa quran ni kitabu imara na cha milele, kiasi kwamba kupita kwa wakati hakuwezi kupunguza hata chembe thamani na itibari ya kitabu hicho. 

Ifuatayo sasa ni aya ya 3 ya sura hiyo ambayo inasema:

"Bila shaka Mola wenu ni Mwenyezi Mungu ambaye ameziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Arshi. Yeye ndiye anayepitisha mambo yote. Hakuna muombezi ila baada ya idhini yake. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu, basi Muabuduni yeye. Je hamkumbuki?"  

Moja kati ya taratibu alizojiwekea Mwenyezi Mungu sw ni kuumba ulimwengu hatua kwa hatua. Na ndiyo maana pamoja na kuwa na uwezo wa kuuumba ulimwengu na kila kiumbe wakati mmoja, Allah sw aliamua kuziumba mbingu na ardhi katika nyakati sita tofauti. Na hivyo ndivyo alivyojaalia pia katika maumbile ya viumbe wengine akiwemo binaadamu ambaye pia uumbwaji wake ni wa hatua kwa hatua, toka tone la manii, pande la damu na hadi mwishowe kufikia kiumbe kamili. Kama tunavyoona kitoto kichanga kabla ya kuja duniani hupitisha kipindi cha miezi tisa tumboni mwa mama kikiwa katika umbo na hali tofauti hadi kuwadia wakati wa kuja duniani, hali ya kuwa kama angetaka, yeye Mola aliye Muweza wa kila kitu angeufanya uumbaji wote huo katika lahadha moja tu. Baadhi ya yale tunayojifunza katika aya hii ni kuwa uumbaji wa ulimwengu umetokana na ratiba na wakati maalumu na si jambo lililotokea kwa sadfa tu. Aidha aya inatuonyesha kuwa ulimwengu ni kitu kinachofuata kanuni na malengo maalumu. Na sababu ni kuwa mumbaji wake ni mmoja tu. Darsa hii ya 306 inahitimishwa na aya ya 4 ambayo inasema:

"Kwake ndiyo marejeo yenu nyote. Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli. Hakika yeye ndiye aliyeanzisha viumbe na ndiye atakayewarejesha (baada ya kufa kwao) ili awalipe kwa uadilifu wale walioamini na kufanya vitendo vizuri. Na wale waliokufuru wao watapata vinywaji vya maji yanayochemka na adhabu inayoumiza kwa sababu ya kukataa kwao."

Aya iliyotangulia imeashiria uwezo wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa mbingu na ardhi. Aya hii ya nne inazungumzia uumbaji wa mara ya pili wa viumbe, yaani kufufuliwa kwao siku ya kiyama; na katika kuliondolea shaka suala hilo inasema, hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu isiyo na shaka ambapo wale waliomwamini Mola wao wakatenda mema watapata jaza ya kheri, na wale waliomkufuru, malipo yao yatakuwa ni adhabu. Tabaan yote hayo yatafanyika kwa uadilifu ambayo ni miongoni mwa sifa kuu za Allah sw. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hii ni kuwa falsafa ya kufufuliwa viumbe ni kuthibiti kwa uadilifu wa Mwenyezi Mungu mtukufu. Kwani dunia hii ndogo na ya kupita tunayoishi haitoshi kuwa ni mahali pa kuwalipa kiadilifu wale waliomwamini Allah na kutenda mema na pia kuwapa adhabu wanayostahiki wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu na kufanya kila aina ya dhulma. Aidha aya inatuelimisha kuwa kama dunia na kila kilichomo ndani yake kimeumbwa kwa ajili ya mwanaadamu, huko akhera pia kuwepo kwa ulimwengu huo na neema na nakama zake vitakuwepo kwa ajili ya kutoa malipo kwa sisi wanadamu kutokana na yale yaliyotangulizwa na mikono yetu. Darsa ya 306 imefikia tamati. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa na mwisho mwema na kutunusuru na adhabu ya moto. Amin.