kisa cha Isra na Miraj
Aya 1: Israi
Maana
Ametakasika aliyempeleka usiku mja wake kutoka Msikiti Mtakatifu mpaka msikiti wa mbali ambaotumevibariki vilivyo kandoni mwake, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
Maana
Maana ya neno Israi katika lugha ya kiarabu ni kutembea usiku. Makusudio ya neno ‘mja wake’ hapa ni Muhammad (s.a.w.). Msikiti mtak- tifu ni ule ulioko Makka kwenye Al-ka’ba.
Anasema mwenye Rawhul-lbayan na wengineo: “Riwaya iliyo sahihi zaidi ni kuwa safari ya Israi ilianzia kwenye nyumba ya Ummu Hani, dada yake Ali bin Abu Twalib.”
Msikiti wa mbali (Masjidul-Aqswa) ni hekalu la Nabii Suleiman. Umeitwa msikiti kwa sababu ni mahali pa kusujudu, kutokana na neno la Kiarabu masjid (msikiti) lenye maana ya mahali pa kusujudu. Na umeitwaMasjidul Aqswa (msikiti wa mbali), kwa sababu ya kuwa mbali na Makka. Msikiti huo umebarikiwa kandoni mwake kwa baraka za kidini, kwa vile ni nchi ya mitume na kwa baraka za kidunia kwa mito na miti.
Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
Inawezekana ‘Yeye’ kuwa ni Mwenyezi Mungu kwa maana ya kuwa anamjua Mwenye kuamini na mwenye kukanusha tukio la Israi. Pia inawezekana kuwa ‘yeye’ hapa ni Muhammad (s.a.w.) kwa maana ya kuwa anajua ukuu na utukufu wa Mwenyezi Mungu.
Imesemekana kuwa Israi ilikuwa usiku wa kuamkia tarehe 27 Rajab (mfunguo kumi). Na pia imesemekana ilikuwa 17 Rabiul-awwal (mfunguo sita).
Israi Kwa Roho Na Mwili
Ulama wengi wanalitumia neno israi kwa safari ya Mtume (s.a.w.) kutoka Masjidul-haram (Msikiti Mtukufu) ulioko Makka, hadi Masjidul-aqswa (Msikiti wa mbali) ulioko Baytul- muqaddas (Nyumba yenye kutakaswa).
Na wanalitumia neno Mi’raj (miraji) kwa safari ya kutoka Baytul-muqad- das hadi juu mbinguni. Wengine hawatofautishi baina ya maneno hayo mawili; wanatumia Miraji kwa kupanda mbinguni na Israi kwa kutoka Makka hadi Baytul-Muqaddas1.
Wote wameafikiana kutokea tukio hili kutokana na nukuu za Qur’an na Hadith za Mtume. Lakini wametofautiana kuwa je, lilikuwa kwa roho tu bila ya mwili au kwa mwili na roho? Sisi tuko pamoja na wale wasemao lilikuwa kwa mwili na roho. Hapa tutazungumzia Israi – safari ya kutoka Msikiti Mtakatifu hadi Msikiti wa mbali. Ama miraji - kupanda juu mbin- guni, mazungumzo yake yatakuja katika Juz. 27 Sura 53.
Wale wanaosema kuwa ilikuwa ni kwa mwili na roho wametoa dalili zifuatazo:
1. Israi ni jambo linaloingia akilini na dhahiri ya wahyi umelitolea dalili; pale aliposema Mwenyezi Mungu: “Aliempeleka usiku mja wake” na hakusema roho ya mja wake. Neno mja linatumika kwa roho na mwili; kama alivyosema Mwenye Mungu:
“Je, unamuona yule ambaye anamkataza mja anaposwali?” (92: 10). Misingi (usul) ya Uislamu iliyothibitishwa ni kuwa kila lililoelezwa na dhahiri ya wahyi na lisipingane na akili, basi ni lazima kuliamini.
Kama Israi ingelikuwa ni kwa roho tu, kusingelikuwa na mshangao wowote, wala washirikina wasingeliharakisha kumfanya mwongo Muhammad. Kuna Hadith isemayo kuwa Ummu Hani alimwambia Mtume mtukufu (s.a.w.): “Usiwaambie watu wako hilo, nahofia watakufanya muongo,” lakini hakutilia maanani hofu ya Ummu Hani kwa kuona kuwa maadamu ni haki basi haina neno. Kwa hiyo akawatangazia watu wake aliyoyaona. Wakashangaa na wakampinga. Kama ingelikuwa ni kwa usingizi wasingelikuwa na mshangao huu.
2. Kwenda Israi kimwili na kiroho ni nembo ya kuwa kila mtu ni lazima ayafanyie kazi maisha yake ya kimwili na kiroho, sio upande mmoja tu.
3. Ni mashuhuri kuwa Mtume amesema: “Nilipelekwa usiku kwenye mnyama anayeitwa Buraq.” Ni wazi kwamba Israi ya kiroho peke yake haihitajii kupanda mnyama wala chombo chochote.
Kwa mnasaba wa Buraq tutaashiria makala iliyo kwenye gazeti la Al-Jumhuriya la Misr, iliyoandikwa na Muhammad Fathi Ahmad, yenye kichwa cha maneno ‘Madhumuni ya kisayansi ya Israi na Miraji,’ Ninamnukuu:
“Alipanda Mtume mtukufu mnyama anayeitwa Buraq. Kulingana na Hadith ni mnyama anayemzidi punda kwa kimo na yuko chini kidogo ya baghala. Hapo kuna somo kutoka kwa Mwenyezi Mungu tunapaswa tulitafutie maelezo Mwenyezi Mungu hashindwi kumchukua Mtume wake kutoka Makka hadi Baytul-Muqaddas bila ya nyenzo yoyote ambapo Mtume angeweza kujikuta tu yuko kwenye mlango wa Masjidul-aqswa. Lakini Mwenyezi ambaye imetukuka hekima yake alipitisha kuwa kila kitu kiende kwa kanuni yake, bila ya mabadiliko wala mageuko.
Safari hii iliyokata masafa marefu katika kasi ya kushangaza, inahimiza akili ianzishe nyenzo mpya ya kwenda masafa marefu katika muda mdogo. Kisha tujiulize, ni kitu gani katika ulimwengu kinakwenda kasi zaidi kulin- gana na utafiti wa elimu? Bila shaka jibu litakuja bila ya kusita kuwa ni mwangaza ambao unakwenda kwa kasi ya 300,000 km. kwa sekunde moja.
Buraq aliyemtumia Mtume alitembea kwa kasi ya mwanga kwa sababu neno Buraq ni mnyambuliko wa nenoBarq lenye maana ya mwako kama wa umeme (flush).
Kupitia majaribio ya kiakili katika uchunguzi wa anga za juu, binadamu ameweza kugundua siri nyingi na ameweza kwa nguvu ya elimu kupenya kutoka ardhini hadi kwenye ufalme wa mbingu. Lakini elimu ya maada pekee inamsahaulisha binadamu na muumba wake.
Tukio la Israi na Miraji linatupa somo kwamba maada na roho ziko sambamba. Kwa hiyo kwenda kwake kwenye utukufu wa juu kulikuwa ni kwa umbile la kibinadamu kutokana na maada na kuendeshwa kulikotokana na roho ya Muumba Mtukufu. Jibril akawa anachukua nafasi ya muelekezaji njia. Nasi hatuna kizuizi cha kumfanya ni nembo, kwa madaraka ya elimu, ambayo itatuongoza kwenye safari yetu katika maisha haya kuelekea kwa muumba wa ulimwengu”.
Ya kushangaza niliyoyasoma kuhusu maudhui haya ni kauli ya anayesema kuwa Israi ya Mtume (s.a.w.) ilikuwa kwa roho sio kwa mwili wake mtukufu kwa kutoa dalili ya hadith iliyopokewa kutoka kwa Aisha, kwamba mwili wa Mtume haukumwacha usiku ule. Na inajulikana kuwa wakati wa Israi, Aisha alikuwa mdogo, wala hakuwa ameolewa na Mtume (s.a.w.). Kwa hiyo Hadithi hiyo inajipinga yenyewe.
Masjidul-Haram Na Masjidul-Aqswa
Masjidul-Aqswa unafanana na Masjidul-Haram katika mambo haya yafutayo:-
1. Yote iko upande wa mashariki.
2. Historia ya yote ni ya zamani; isipokuwa Masjidul-haram ni wa zamani zaidi na pia ni mtukufu zaidi. Kwa sababu ndiyo nyumba ya kwanza kujengwa kwa ajili ya ibada duniani: “Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu ni ile iliyoko Makka yenye kubarikiwa na mwongozo kwa viumbe. Mna humo ishara zilizo wazi: Mahali aliposimama Ibrahim. Na mwenye kuingia humo huwa katika amani; na ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya watu kuhiji nyumba hiyo kwa mwenye kuweza njia ya kuiendea. Juz. 4 (3:96–97).
3. Miji yote miwili, Makka ulio na Masjidul-haram na mji wa Quds ulio na Msjidul–Aqswa ilianzishwa na Waarabu au walishiriki kuianzisha. Makka ilijengwa na Ibrahim na mwanawe Ismail waliojenga Al-ka’aba: “Na tuliagana na Ibrahim na Ismail kuwa: Itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wenye kutufu na wenye kujitenga huko kwa ibada na wanaorukuu na kusujudu… Na Ibrahim alipoinua misingi ya ile Nyumba (Al-Kaaba) na Ismail (wakaomba): Ewe mola wetu! Tutakabalie; hakika wewe ndiye Msikizi, Mjuzi.” Juz. 1(2: 125, 127).
Inajulikana kuwa Ismail ndiye Mtume wa kwanza kuzungumza lugha ya Kiarabu ambayo haikuwa lugha ya baba yake. Maquraysh na waarabu wengineo wanatokana naye. Qur’an ilishuka kwa lugha yake.
Quds nayo waliishi hapo wayabusi, kabila la waarabu wa Kanani. Walifika kwenye mlima maarufu unaojulikana kwa jina la Zayuni, mnamo mwaka wa 2500 (B.C.) kabla ya kuzaliwa Nabii Isa wakiongozwa na mzee wao aliyeitwa Salim Al-yabusi. Watu wa kabila hili ndio wa kwanza kuweka jiwe la kwanza la kujenga mji wa Quds ambao baadae ulikuwa ndio Qibla cha ulimwengu.2
Baada ya Waislamu kuuteka mji wa Quds walijenga msikiti ulioitwa Masjid Umar, uliasisiwa na Umar bin A-khattwab na Masjid Qubbatusswakhra (msikiti wa kuba la mwamba) ulioasisiwa na Abdulmalik bin Marwana. Yote hiyo ilikuwa ndani ya haramu ya Quds. Waislamu walikuwa hawaruhusu asiyekuwa Mwislamu kukanyaga hapo.
4. Waislamu wanaitukuza misikiti yote miwili, ambapo mwanzo walikuwa wakiswali kwa kuelekea Masjiul-Aqswa kwa muda wa miaka 13 wakiwa Makka na miezi kadhaa Madina. Kuongezea safari ya Israi, inakuwa si jambo la ajabu kwa Waislamu kupafanya mahali hapo ni pa takatifu na ni pa pili baada ya Makka na Madina kwa utukufu, heshima na ulinzi.
Mpokezi mengi yanaeleza kuwa Mtume alimfunga Buraq hapo Baytul-Muqaddas. Mpaka sasa ukuta wa magharibi ya haram, mahali alipomfunga, unaitwa ukuta wa Buraq, pia mapokezi yanaeleza kuwa Mtume aliswali kwenye sehemu ya mwinuko katika hekalu la Nabii Suleiman, pamoja na Nabii Ibrahim, Musa na Isa akiwa yeye ndiye Imam. Na kwamba yeye alitumia mwamba wa Ya’qub kuwa ndio kituo chake cha kupanda mbinguni.
Ndio maana uharibifu wa Quds mnamo mwaka 1967 uliyotekelezwa na wazayuni na wakoloni wa kimarekani na waingereza, ni maafa ya waislamu na wakiristo.
Mkono mchafu ulichafua na kudharau sehemu takatifu za dini ya kiislamu na ya kikiristo. Usiku huo wa damu walikesha na ufuska; wakafanya sherehe za dansi na ulevi.
Ajabu ya maajabu ni kwa Marekani na Uingereza kudai kuwa wao ni wahami wa dini na ni maadui wa ulahidi, wakati huo huo wakiwasaidia wazayuni amabo hawaamini misimamo yoyote, hawaheshimu maadili, hawaheshimu dini za wengine wala hawatambui haki yoyote katika haki za binadamu.
Amerika na Uingerza zimeisaidia Israili, zikaipa mali na silaha na zikaiunga mkono kweneye Baraza la usalama na Umoja wa mataifa. Zikaipongeza kwa kuingila sehemu takatifu za waislamu na wakiristo. Wameendelea na misimamo hii ulimwenguni pote.
Sisi hatuna shaka kwamba iko siku itawafikia wakoloni na marafiki zao wazayuni kupitia mikononi mwa wanamapinduzi wapigania uhuru; kama ilivyowafikia hivi sasa wamarekani kutoka kwa wavietnam na kabla yake iliwafikia wazayuni kutoka kwa Nebuchadnezzar, Waroma, Mtume (s.a.w.) na Khalifa wa pili Umar bin Al-khattwab.
Hivi sasa kila siku vyombo vya habari haviachi kutangaza habari za upinzani wa Palestina na kujitoa mhanga ambako kumeifanya Israil yote iishi kwenye jinamizi la hofu na woga.3
Somo Katika Israi
Qur’an hii ambayo tunaisoma ni masomo aliyompatia Muumbaji Mtume wake ili ayafikishe kwa watu wote. Masomo haya yako aina nyingi. Miongoni mwayo ni hukumu ya maarifa ya halali na haramu, jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, ikhlasi na subira kwa ajili ya haki.
Lililo muhimu zaidi katika yote ni kumwamini Mwenyezi Mungu na utukufu wake kwa imani sahihi inayobainishwa na maarifa ya kujua; sio kwa kuigiza, kasema fulani au kwa kuwazia tu.
Mwenyezi Mungu ameongoza njia za elimu na yakini ambazo ni kufikiri katika maumbile ya ulimwengu pamoja na ardhi na mbingu yake. Pia mipangilio, hekima na mfumo sahihi katika vyote vilivyo baina ya mbingu na ardhi, vikiwa mbalimbali na pamoja:
أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا فِي أَنْفُسِهِمْ ۗ مَا خَلَقَ اللَّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَأَجَلٍ مُسَمًّى ۗ {8}
“Hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi ila kwa haki na kwa mudamaalum.” (30:8).
Baada ya Mwenyezi Mungu kumpa wahyi mja wake kwa somo la ukuu wa ulimwengu na kuumba mbingu na ardhi, alimuhusisha yeye tu kwa safari ya ardhini, kutoka Masjidul-haram hadi Masjidul-aqswa na safari ya mbinguni, kutoka Masjidul-aqswa hadi kwenye wingu wa juu.
Lengo la safari hizi mbili ni kuwa Mtume apate somo la kimatendo baada ya kupata la kinadharia kuhusu ulimwengu, aone mwenyewe, kwa macho yake, maajabu ambayo akili haiwezi kuyawazia. Njia hii, siku hizi, watu wanaifuata, ambapo waalimu wanawaandalia wanafunzi wao safari za kimasomo ili wakajionee wenyewe yale waliyojifunza.
Kwa hiyo basi somo kubwa katika safari mbili za Mtume ni kuhimiza akili kuangalia vizuri katika uumbaji wa mbingu na ardhi:
أَوَلَمْ يَنْظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّهُ مِنْ شَيْءٍ {185}
“Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na alivyoviumba Mwenyezi Mungu.” Juz. 9 (7:185).
Imam Ali (a.s.) anasema: “Nashangaa na anyemtilia shaka Mungu na anaona alivyoviumba Mungu!”
وَآتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَجَعَلْنَاهُ هُدًى لِبَنِي إِسْرَائِيلَ أَلَّا تَتَّخِذُوا مِنْ دُونِي وَكِيلًا {2}
Na tukampa Musa Kitabu na tukakifanya ni uongofu kwa Wana wa Israil, kwamba msi- fanyemtegemewa asiyekuwa Mimi.
ذُرِّيَّةَ مَنْ حَمَلْنَا مَعَ نُوحٍ ۚ إِنَّهُ كَانَ عَبْدًا شَكُورًا {3}
Enyi kizazi tulichokichukua pamoja na Nuh! Hakika yeye alikuwa ni mja mwenye shukrani.
· 1.Waswahili wamezoweya kutumia neno Miraji kwa safari yote ya kutoka Makka hadi mbinguni kupitia Baytul - Muqaddas - Mtarjumu.
· 2.Maelezo hayo yanatokana na uchambuzi wa mtaalam Michel Khalil, uliotolewa na jarida la Al-yawm no. 25/5/1968
· 3.Kumbuka mazungumzo haya ni ya miaka ya sitini