Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
HISTORIA YA WATUKUFU

FATIMA MAMA MTUKUFU

2018/02/04

FATIMA MAMA MTUKUFU

Fatima Az-Zahrau Mama Wa Maimam Watakasifu

Nasaba Yake Tukufu

Hakika kiungo kati ya uimamu na utume ni Fatima binti Muhammad, mama wa Maimam maasumina na mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni. Mama yake ni mbora wa wanawake wa kikuraishi, Khadija binti Khuwaylid bin Asad bin Abdul-Uzza bin Quswayy, na yeye ndiye mke wa kwanza wa Mtume (s.a.w.w.) na yeye alitokana na nyumba yenye elimu na sharafu. Hakika kumzaa mtu kama Fatima Az-Zahrah mkweli, mtakasifu na maasumu kunatosha kabisa kuwa utukufu mkubwa kwake.

Mazazi Yake Matukufu

Tabarasiy ndani ya kitabu Iilamul-Waraa amesema: “Linalodhihiri katika riwaya za wapokezi wetu ni kuwa alizaliwa Makka siku ya ishirini ya mfungo tisa mwaka wa tano tangu Mtume (s.a.w.w.) kukabidhiwa utume, na Mtume (s.a.w.w.) alifariki Fatima akiwa na umri wa miaka kumi na nane na miezi saba.”1

Imepokewa kutoka kwa Jabir bin Yazid kuwa alisema: “Imam Al- Baqir (a.s.) aliulizwa: Fatima aliishi muda gani tangu kufariki kwa Mtume (s.a.w.w.)? Akajibu: “Miezi minne na akafariki akiwa na umri wa miaka ishirini na tatu.”2

Hakika hili linakaribiana sana na yale waliyoyapokea wasiokuwa Imamiya kuwa alizaliwa mwaka wa arubaini na moja tangu kuzaliwa Mtume (s.a.w.w.), hivyo atakuwa kazaliwa mwaka mmoja tangu Mtume (s.a.w.w.) kukabidhiwa utume.3

Mwalimu wetu Abu Said Al-Waidhiy ndani ya kitabu Sharafun-Nabii amesema: “Watoto wote wa Mtume (s.a.w.w.) walizaliwa kabla ya Uislamu isipokuwa Fatima na Ibrahim hakika wao wawili walizaliwa ndani ya Uislamu.”4

Majina Yake Na Lakabu Zake

Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar As-Sadiq (a.s.) kuwa alisema: “Fatima ana majina tisa mbele ya Mwenyezi Mungu: Fatima, As- Siddiqah, Al-Mubarakah, At-Tahirah, Az-Zakiyyah, Ar-Radhiyah, Al- Mardhiyyah, Al-Muhaddathah na Az-Zahrau.”5

Imepokewa kutoka kwa Imam Ridha (a.s.) kuwa Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Hakika binti yangu amepewa jina la Fatima kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtenga mbali na moto yeye na yule atakayempenda.”6

Mtume (s.a.w.w.) alimpa jina la Batul7 kisha akamwambia Aisha: “Ewe mwenye macho mekundu, hakika Fatima si kama wanawake wa kibinadamu yeye hapatwi na siku kama mnavyopatwa na siku.”8

Alikuwa akichuruzika maji ya Peponi kwa sababu pindi Mtume (s.a.w.w.) alipopelekwa miraji aliingia Peponi akala na kunywa chakula na maji ya Peponi kisha usiku huo huo akarudi na kumwingilia mkewe Khadija na akawa kashika mimba ya Fatima, hivyo mimba ya Fatima ikatokana na maji ya Peponi.9

Makuzi Yake

Fatima amezaliwa na kutokana na wazazi wawili watukufu, kwani hakuna mtu yeyote ambaye ana baba mwenye athari kama za baba yake, athari ambazo zilibadili sura nzima ya historia, huku ndani ya muda mfupi zikimpeleka mwanadamu hatua za mbali kuelekea mbele.

Wala historia haijatusimulia kuhusu mama kama mama yake ambaye alimpa mume wake na dini yake tukufu kila alicho nacho kwa malipo ya kupata uongofu na nuru.

Chini ya kivuli cha wazazi hawa wawili watukufu ndipo alipokulia Fatima Al-Batul, akakulia ndani ya nyumba ambayo imezungukwa na mapenzi ya baba yake ambaye alibeba joho la utume na akavumilia yale ambayo majabali yalishindwa kuvumilia.

Vipindi Vya Maisha Yake

Fatima Az-Zahrau (a.s.) aliishi ndani ya misukosuko ya kufikisha ujumbe tangu utotoni mwake, akawekewa vikwazo yeye, baba yake, mama yake na Bani Hashim wengine katika bonde maarufu ilihali wakati vikwazo vinaanza alikuwa hana umri isipokuwa miaka miwili tu.

Vilipoondolewa tu vikwazo baada ya miaka mitatu migumu akakum- bana na msukosuko mwingine nao ni kufiwa na mama yake kisha kufariki ami yake huku akiwa mwanzoni mwa mwaka wake wa sita, hivyo akabakia kama kifuta machozi cha baba yake akimliwaza wakati wa upweke huku akimsaidia dhidi ya majeuri na mabeberu ya kikurayshi.

Mtume akahama kuelekea Madina yeye na Fatima mwingine akiwa ni mtoto wa ami yake Ali (a.s.) huku akiwa na umri wa miaka minane, hivyo akabakia na baba yake mpaka alipokutanishwa na mtoto wa ami yake, Ali bin Abu Twalib, hapo ikaanzishwa nyumba tukufu ndani ya Uislamu kwani Fatima aligeuka chombo safi cha kuendeleza kizazi kitakatifu cha Mtume (s.a.w.w.) na kheri nyingi waliyopewa kizazi kitakasifu cha Mtume (s.a.w.w.).

Az-Zahrau alitoa mfano bora wa mke na mama ndani ya kipindi kigumu cha historia ya Uislamu, kipindi ambacho Uislamu ulikuwa unataka kuweka njia ya kudumu ya utukufu wa juu lakini ndani ya mazin- gira ya kijahiliya na mila za kikabila zinazokataa uwanadamu wa mwanamke huku zikimhesabu mwanamke kuwa ni aibu.

Hivyo ikawajibika kwa Az-Zahrau kutumia mwenendo wake binafsi na wa kijamii ili kuwa mfano halisi wa kivitendo unaojenga mjengo halisi wa mafunzo na hadhi ya ujumbe wa Mwenyezi Mungu.

Az-Zahrau ameuthibitishia ulimwengu wa wanadamu kuwa yeye ni mwanadamu timilifu ambaye ameweza kuwa alama ya uwezo wa juu wa Mwenyezi Mungu na muujiza wake wa ajabu, hiyo ni kutokana na hadhi, heshima na utukufu aliokuwa nao. Az-Zahrau Al-Batul alimzalia Ali (a.s.) watoto wawili watukufu wa kiume nao ni mabwana wa vijana wa Peponi na watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu: Hasan na Husein Maimam watakasifu, pia alimzalia mabinti wawili watukufu: Zaynabu mkubwa na Ummu Kulthum wapiganaji wawili wenye subira.

Az-Zahrau alimporomosha mwanae wa tano Muhsin baada ya kifo cha baba yake kutokana na matukio ya uadui dhidi ya nyumba yake, nyumba ya utume na uimamu, hapo zikatimia habari za Qur’ani ili- posema:

“Hakika sisi tumekupa kheri nyingi.* Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje.* Hakika adui yako atakuwa mkiwa.”

Hivyo yeye Zahrau ndio kheri nyingi ya utume ambayo Mwenyezi Mungu alimpa Mtume wake (s.a.w.w.), isipokuwa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa anahitaji wenye kujitolea atakaowatoa kwa ajili ya mti wake wenye kustawi ili kuwazima maadui zake ambao tangu mwanzo walisimama kidete kuuwa Uislamu na alama zake.

Kifo Chake Na Kuoshwa Kwake

Az-Zahrau (a.s.) alifariki Madina siku ya tatu ya mfunguo tisa mwaka wa kumi na moja. Aliishi siku tisini na tano tangu kufariki kwa Mtume (s.a.w.w.).10 Wengine wamepokea kuwa aliishi miezi minne. Wengine wakasema siku arubaini. Pia imepokewa kuwa aliishi siku sabini na tano huku wengine wakidai aliishi miezi sita au minane.11

Imam Ali (a.s.) ndiye aliyemwosha.12 Imepokewa kuwa Asmaa binti Umays ndiye aliyemsaidia Imam Ali (a.s.) kumwosha. Az-Zahrau alikuwa kaacha usia kuwa atakapofariki asioshwe na yeyote yule isipokuwa Ali (a.s.) na Asmaa.13

Mazishi Yake Na Eneo La Kaburi Lake

Aliswaliwa usiku, na waliomswalia ni Ali (a.s.), Hasan, Husein, Ammar, Mikdad, Aqil, Zubeyr, Salman, Baridah na kundi dogo la Bani Hashim. Kisha kiongozi wa waumini Ali (a.s.) akaenda kumzi- ka kwa siri ikiwa ni kutekeleza usia wake kuhusu hilo.14

Watu wametofautiana kuhusu eneo la kaburi lake, yupo anayesema kuwa alizikwa Baqii.15 Yupo anayesema alizikwa nyumbani kwake. Bani Umaiyya walipozidi msikitini ikawa ni msikitini.16

Yupo anayesema kuwa alizikwa kati ya kaburi la Mtume (s.a.w.w.) na mimbari yake.17 Huenda hili ndilo lililoashiriwa na Mtume (s.a.w.w.) aliposema: “Kati ya kaburi langu na mimbari yangu kuna kiunga kati ya viunga vya peponi.”18 Isipokuwa Tabarasiy amesema: “Kauli ya kwanza iko mbali na usahihi, na kauli mbili za mwisho zinakaribia usahihi, hivyo anayechukua tahadhari katika kumzuru humzuru mae- neo yote matatu.”19

Muhtasari

Fatima Az-Zahrau (a.s.) mbora wa wanawake wote na binti wa mbora wa viumbe amekulia chini ya kivuli cha nabii wa rehema na mlezi wa wanadamu, hivyo Mwenyezi Mungu akampenda kutokana na sifa zake bora. Mama yake alifariki huku akipambana na misukosuko kwa ajili ya ujumbe wa Mwenyezi Mungu, hivyo Fatima (a.s.) akawa kifuta machozi na liwazo la baba yake.

Alihama kutoka Makka akiwa na mtoto wa ami yake ili aungane na baba yake ambaye alikuwa ameanza kujenga misingi ya dola ya kiislamu iliyobarikiwa.

Mwenyezi Mungu alimteua awe mke wa Ali bin Abu Twalib, hivyo akatoa mfano bora wa mwanamke wa kiislamu, huku akiwa ni chombo safi cha kuendeleza kizazi cha Mtume (s.a.w.w.) ambacho kiliendelea kupitia wanae wa kiume mabwana wa vijana wa Peponi, hivyo yeye akawa ni makutano ya utume na uimamu.

Aliishi na baba yake na mumewe ndani ya matatizo yote ya ulinganio wa Uislamu akashirikiana nao katika jukumu la kujenga Uislamu.

Baada ya baba yake alikumbana na dhulma toka kundi lililoacha njia, hivyo akaporomosha (kuharibika mimba) mwanae wa tano kutokana na tukio la uadui alilofanyiwa yeye pamoja na mumewe. Baada ya tukio hilo hakuishi muda mrefu akawa ameungana na baba yake huku akiwa mwenye subira mvumilivu wa maudhi yote yaliyomfika kwa ajili ya ujumbe wa milele wa Muhammad (s.a.w.w.).

Maswali

1. Fatima Az-Zahrau amezaliwa wapi? 2. Pindi Mtume (s.a.w.w.) alipokabidhiwa utume Fatima (a.s.) alikuwa na umri wa miaka mingapi? 3. Fatima Az-Zahrau aliolewa lini? 4. Ni watoto gani wa kiume na wa kike waliozaliwa na Fatima? 5. Ni vipi vipindi vya maisha yake? 6. Kwa nini nyumba ya Fatima Az-Zahrau ndio nyumba tukufu ndani ya Uislamu? 7. Lini, wapi na vipi alizikwa Az-Zahrau (a.s.)?

·         1. Iilamul-Waraa, Juz. 1, Uk. 290.

·         2. Mfano wa hiyo inapatikana ndani ya kitabu Manaqib cha Ibnu Shah’ri Ashuub, Juz. 1, Uk. 357.

·         3. Mustadrakul-Hakim, Juz. 3, Uk. 161 na 163. Al-Istiab, Juz. 4 Uk. 374. Maqtal cha Al-Khawarazimiy, Uk. 83. Al-Iswabah, Juz. 4 Uk. 377.

·         4. Iilamul-Waraa, Juz. 1, Uk. 290.

·         5. Amalis-Suduq, Uk. 484. Al-Khiswal, Juz. 2, Uk. 414. Dalailul-Imamah, Uk. 10. Tajul-Mawalid, Uk. 20.

·         6. Uyunu Akhbar-Ridha, Juz. 2 Uk. 46. Maanil-Akhbar, Uk. 64. Ilalus- Sharaiu, Uk. 178.

·         7. Ilalus-Sharaiu, Uk. 181. Manaqib cha Ibnu Shah’ri Ashuub, Juz. 3, Uk. 330.

·         8. Manaqib cha Ibnu Shah’ri Ashuub, Juz. 3 Uk. 330. Al-Muujam Al- Kabir, Juz. 22, Uk. 400.

·         9. Rejea aliyoyapokea Ibnu Abbas kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) ndani ya kitabu Manaqib cha Ibnu Al-Mughazaliy, Uk. 357 na 406. Manaqib cha Al- Khuwarazamiy, Uk. 64. Dhakhairul-Uqba, Uk. 36.

·         10. Adh-Dhuriyat-Tahirah cha Ad-Duulabiy, Uk. 151 na 199. Kashful- Ghummah, Juz. 1, Uk. 503.

·         11. Manaqib cha Ibnu Shah’ri Ashuub, Juz. 3 Uk. 357. Al-Iswabah, Juz. 4, Uk. 379. Jalaul-Uyun, Juz. 1, Uk. 216.

·         12. Al-Kafiy, Juz. 1, Uk. 382. Ilalus-Sharaiu, Uk. 184. Dalailul-Imamah, Uk. 46. Tajul-Mawalid, Uk. 98. Al-Istiaab, Juz. 4, Uk. 379.

·         13. Kashful-Ghummah, Juz. 1, Uk. 500. Mustadrakul-Hakim, Juz. 3, Uk.163. Al-Istiaab, Juz. 4, Uk. 379.

·         14. Rawdhatul-Waidhina, Uk 152. Tajul-Mawalid, Uk. 98. Manaqib cha Ibnu Shah’ri Ashuub, Juz. 3, Uk. 363. Sahih Bukhari, Juz. 5, Uk. 177. Sahih Muslim, Juz. 3, Uk. 1380. Tabaqat cha Ibnu Saad, Juz. 8 Uk. 229 Muswannaf cha Abdur-Razzaq, Juz. 5 Uk. 427. Sunan Al-Bayhaqiy, Juz. 6, Uk. 300. Tarikh At-Tabariy, Juz. 3, Uk. 208. Mustadrakul-Hakim, Juz. 3 Uk. 162. Al-Istiaab, Juz. 4, Uk. 379. Usudul-Ghaba, Juz. 5, Uk. 524.

·         15. Tajul-Mawalid, Uk. 99. Manaqib cha Ibnu Shah’ri Ashuub, Juz. 3, Uk. 357. Kashful-Ghummah, Juz. 1, Uk. 501.

·         16. Al-Kafiy, Juz. 1, Uk. 383. Al-Faqihi, Juz. 1, Uk. 148. Uyunul-Akhbar- Ridha, Juz. 1, Uk. 311. Maanil-Akhbar, Juz. 1, Uk. 268. Dhakhairul-Uqba Uk. 504.

·         17. Maanil-Akhbar, Juz. 1, Uk. 268. Rawdhatul-Waidhina, Uk. 152.

·         18. Al-Kafiy, Juz. 4, Uk. 553-555. Al-Faqihi, Juz. 2 Uk. 339. At-Tahdhib cha Tus, Juz. 6, Uk. 7. Al-Muwatta, Juz. 1, Uk. 97. Sahih Bukhar, Juz. 2, Uk. 77. Sahih Muslim, Juz 2, Uk. 1010. Musnad Ahmad, Juz. 2, Uk. 236 na 376 na 438 na 466 na 533. Pia Juz. 3, Uk. 4, na Juz. 4, Uk. 39 na 40. Sahih Tirmidhiy, Juz. 5, Uk. 718 na 719. Sunan An-Nasaiy, Juz. 2, Uk. 35

·         19. Iilamul-Waraa, Juz. 1, Uk. 293.