SERIKALI YA MTUE (S.A.W.W)
SERIKALI YA MTUME (S.A.W.W)
IMEANDIKWA NA: BARAZA
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
Ushahidi na nyaraka za historia za kabla ya kudhihiri Uislamu zinaonyesha kuwa hakukuwepo utawala na serikali katika ardhi ya Hijaz na kwamba maisha ya Waarabu wa jangwani hayakutawaliwa na mfumo makhsusi wa kisiasa. (1) Ni baada ya kudhihiri dini ya Uislamu huko Makka na kuhamia Mtume Muhammad katika mji wa Madina ndipo mtukufu huyo alipoanzisha serikali kuu na kubadili mfumo wa kikabila uliokuwa ukitawala kwa kuasisi mfumo mpya wa kisiasa na kijamii. Mbali na kutoa mafunzo na malezi kwa jamii ya watu wa Hijaz, Mtume Muhammad (saw) pia aliongoza yeye binafsi jamii changa ya Kiislamu na kushika hatamu za mfumo wa kijamii wa Waislamu katika nyanja mbalimbali za sheria, utamaduni, siasa, masuala ya kijeshi na kiuchumi.(2) Suala hilo linaonekana wazi zaidi katika mtazamo wa aya za Qur\'ani na ushahidi wa kihistoria kiasi kwamba hata wataalamu wa masuala ya Mashariki (orientalist) wasiokuwa Waislamu wamelifafanua kwa uwazi zaidi. Msomi wa Kitaliano Fel Lino anasema: Mtume Muhammad (saw) aliasisi dini na dola kwa pamoja na masuala yote hayo mawili yalipanuka na kukuwa sambamba katika kipindi cha uhai wake. (3) Dr. Strotmann anaamini kwamba: Uislamu ni tukio la kidini na kisiasa, kwani muasisi wake mbali na kuwa Mtume alishika hatamu za serikali na alikuwa na utaalamu kamili wa kuongoza serikali". (4) Hata hivyo katika karne za hivi karibuni baadhi ya waandishi (5) wametilia shaka uhakika kwamba serikali ya Mtume Muhammad (saw) ilikuwa serikali yenye uhusiano na wahyi na mafundisho ya Mwenyezi Mungu kutokana na kuathirika kwao na mafundisho ya fikra za kisekulari yanayotilia mkazo kutenganishwa dini na siasa. Waandishi hao wanasisitiza kuwa suala la serikali na uongozi ni suala la kibinadamu lizilokuwa na uhusiano wowote wa dini. Wanadai kuwa Nabii Muhammad (saw) hakuwa kiongozi wa kisiasa wala hakuamrishwa na Mwenyezi Mungu kuunda serikali na kuongoza masuala ya jamii. Kwa msingi huo, kama mtukufu huyo aliunda serikali na kuongoza masuala ya jamii alifanya hivyo kutokana na haja ya jamii hiyo na si wajibu wa kidini kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Ili kuweza kujibu vyema madai hayo, inatupasa kwanza kuchunguza na kuchambua mantiki ya Qur\'ani Tukufu kuhusu nafasi ya Mtume Mtukufu (saw) katika serikali ya Kiislamu. a- Uongozi wa Kisiasa wa Mtume Muhammad (saw) Qur\'ani Tukufu inamtambulisha Mtume Muhammad amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake kuwa ni "aula", na mwenye haki zaidi ya kuingilia masuala ya kimaisha ya watu na mwenye mamlaka juu yao. Aya ya 33 ya suratul Ahzab inasema:
النَّبِيُّ أَوْلَى بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ
"Nabii ana haki zaidi kwa Waislamu kuliko nafsi zao.." . Wasomi na wafasiri wa Qur\'ani Tukufu wanasema kuwa neno "aula" na haki kubwa zaidi ya Mtume kwa waumini kuliko nafsi zao haihusu masuala ya kidini pekee bali inahusu masuala yote ya kidini na kidunia. (6) Wanatia nguvu tafsiri hiyo kwa kutumia yafuatayo: 1- Kutofungamanishwa haki hiyo ya Mtume kwa waumini na jambo makhsusi katika aya iliyotajwa, suala ambalo natija yake ni kwamba aya hiyo inagusa nyanja zote za maisha ya mwandamu ikiwemo medani ya siasa na masuala ya jamii. Kwa msingi huo Mtume Muhammad (saw) alipewa na Mwenyezi Mungu mamlaka ya kusimamia na kuendesha masuala yote ya watu. 2- Hadithi zilizopokelewa kutoka kwa viongozi na Maimamu katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw). Imam Muhammad Baqir (as) anasema: Aya hii iliteremshwa ikizungumzia uongozi na kuendesha masuala ya umma". (7) 3- Sababu ya kuteremshwa aya hiyo. Mtume Mtukufu alipiga mbiu na kuwaamuru Waislamu wajitayarishe kwa ajili ya vita. Baadhi ya watu walimwendea Mtume kwa ajili ya kuwaombea ruhusa ya kutokwenda vitani baadhi ya jamaa zao. Hapa ndipo aya hii ilipoteremshwa ikiwaambia waumini kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ana haki zaidi kwa waumini katika masuala yao yote kuliko hata nafasi zao wenyewe. Kutotaka na maelezo hayo inaeleweka vyema kwamba, amri za masuala ya kijamii zinazotolewa na Mtume, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, zinategemea mamlaka aliyopewa na Mwenyezi Mungu na dini ya Uislamu na si matashi na maamuzi ya kibinadamu. (8) 4- Mtume ndiye aula na anayetungulizwa na Mwenyezi Mungu mbele ya watu wengine katika uendeshaji na kuongoza masuala ya jamii kwa mujibu wa maana tunayopata kutoka kwenye aya iliyotangulia na wala hatanguliwi na mtu mwingine. Kuna aya nyingine za Qur\'ani Tukufu zinazoashiria suala hilo. Kwa mfano aya ya 5 ya suratul Maidah inasema:
إِنَّمَا وَلِيُّكُمُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ وَالَّذِينَ آمَنُواْ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُمْ رَاكِعُونَ
"Kiongozi wenu hasa ni Mwenyezi Mungu, Mtume wake na walioamini ambao husimamisha swala na kutoa zaka hali ya kuwa wamerukuu". Kwa msingi huo, katika mtazamo wa Qur\'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu SW amemtanguliza Mtume wake mbele ya watu wengine na kumpa mamlaka na utawala juu yao. Hivyo basi uongozi wa mtukufu huyo unatokana na uongozi na mamlaka ya Mwenyezi Mungu na si suala la kidunia na linalotokana na matashi ya wanadamu. Mfasiri mkubwa wa Qur\'ani wa zama hizi Allamah Muhammad Hussein Tabatabai Mwenyezi Mungu amrehemu anasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ana mamlaka ya uongozi katika masuala yote ya umma wa Kiislamu kwa ajili ya kuuongoza umma kuelekea kwa Mola Mlezi, kutawala, kutoa maamrisho na kuhukumu baina yao… Mamlaka haya yanatokana na mamlaka ya Mwenyezi Mungu na kwa kufawidhiwa na Mola Muweza". (9) Nukta nyingine muhimu ya kuzingatiwa ni kuwa neno إِنَّمَا (Innama) lililotumiwa mwanzoni mwa aya hiyo ya 55 ya suratul Maidah lina maana ya "peke yake" "ni yeye tu" au "yake tu", kwa maana kwamba mamlaka na kiongozi wenu wa pekee ni Mwenyezi Mungu, Mtume wake na waumini wanaotoa zaka hali ya kuwa wamerukuu. Kwa msingi huo, kwa mujibu wa aya hii, utawala na uendeshaji halali wa masuala ya umma ni ule pekee unaofawidhiwa na Mola Muweza kwa Mtume wake na kadhalika. Natija: Kwa kutilia maanani jumla ya aya hizo za Qur\'ani, tunaweza kuelewa vyema kwamba Mtume Mtukufu alikuwa na vyeo na nafasi tatu kwa wakati mmoja: (10) 1- Uimamu, uongozi wa umma na marejeo ya watu katika masuala ya kidini. (Hashr - 7) 2- Uongozi na usimamizi wa masuala ya kutoa hukumu na kukata kesi baina ya wanadamu. (Nisaa - 65) 3- Uongozi wa masuala ya kisiasa na kijamii. (Maidah - 55, Ahzab - 6) b- Majukumu ya Kijamii ya Mtume Muhammad (saw) Kila moja kati ya kazi tatu za Mtume Mtukufu yaani uimamu na uongozi wa kidini, kukata kesi na hukumu baina ya watu na uongozi wa masuala ya kijamii, yanampa mtukufu huyo majukumu na kazi makhsusi. Aya zinazofuata za Qur\'ani Tukufu zinatoa mifano kadhaa ya majukumu na kazi alizopewa Mtume (saw) na kufawidhiwa na Mwenyezi Mungu kuhusu suala la kuongoza jamii na kuendesha masuala ya umma:
1- فَإِمَّا تَثْقَفَنَّهُمْ فِي الْحَرْبِ فَشَرِّدْ بِهِم مَّنْ خَلْفَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ
"Na ukiwapata katika medani ya vita wakimbize walionyuma yao kwa kuwatia adabu hawa ili wapate kufahamu". (Anfal - 57) Aya hii kwa upande mmoja inaeleza siasa zinazopaswa kutumiwa na umma wa Kiislamu mbele ya maadui wavamizi na wavunjaji wa mikataba na makubaliano, na kwa upande mwingine inaeleza kuwa jukumu la kupanga ratiba, kutayarisha mazingira na vitendea kazi na kutekeleza kimatendo siasa hizo ni wadhifa wa Mtume Muhammad (saw).
2- وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّى يَسْمَعَ كَلامَ اللَّهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ
"Na kama yeyote katika washirikina atakuomba hifadhi, mpe hifadhi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu kisha mfikishe mahala pake pa amani". (Tauba - 6) Kwa mujibu wa aya hii Mtume mtukufu anawajibika kudhamini usalama, amani na uhuru wa washirikina wanaokwenda kwake kwa lengo la kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Yaani Mtume Muhammad ndiye anayesimamia masuala ya amani na usalama wa umma na jamii ya wanadamu tena kwa tafwidhi ya Mwenyezi Mungu. (al Mizan)
3- يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَلَى الْقِتَالِ
"Ewe Nabii! Wahimize waumini wende vitani". (Anfal - 65) Yaani Mtume ndiye mwenye jukumu la kutayarisha majeshi na kuyahimiza kwenda vitani kupigana na maadui.
4 - يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ
"Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanafiki na kuwa shadidi kwao.." (Tauba - 73) Aya hii inampa Mtume (saw) jukumu na mamlaka ya kutayarisha na kuongoza Waislamu kwa ajili ya jihadi na kupambana na washirikina na wanafiki.
5- خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
"Chukua sadaka katika mali zao uwasafishe na uwatakase kwayo.." (Tauba - 103) Kwa mujibu wa aya hii, Mtume amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, ndiye mwenye mamlaka ya kuchukua zaka, ambayo ni aina ya ushuru na kodi ya mapato, kutoka kwa Waislamu. Kwa msingi huo, katika mtazamo wa Qur\'ani, Mtume Muhammad (saw) alipewa jukumu la kuunda serikali na kufawidhiwa uendeshaji wa masuala ya kijamii kutoka kwa Mola Muweza. Ni kwa misngi huo pia ndiyo maana aliunda serikali na kuanzisha dola la Kiislamu mjini Madina. Marejeo: 1- Ulimwengu katika Zama za Kubaathiwa Mtume - Muhammad Jawad Bahonar 2- Dini la Dola katika Fikra za Kiislamu - Muhammad Sorush 3- Mfumo wa Utawala katika Uislamu - Muhammad Yusuf Mussa 4- " " " " " 5- Uislamu na Misingi ya Utawala - Abdulrazaq Ali 6- Tafsiri ya Razi 7- Majmaul Bahrain 8- Majmaul Bayan - Sheikh Tabarsi 9- Tafsiri ya al Mizan - Allama Tababai 10- Kwa ajili ya maelezo zaidi kuhusu vyeo na nafasi ya Mtume Muhammad (saw) na Maimamu watwaharifu katika kizazi chake, tazama kitabu cha Uimamu na Uongozi cha Shahid Murtadha Mutahhari.
MWISHO