Imam Ali bin Abi Talib a.s
Dondoo Za Maisha Ya Mbora Wa Mawasii
Kiongozi Wa Waumini Ali Bin Abu Talib
Baada ya kifo cha nabii wa mwisho Muhammad (s.a.w.w.) uongozi wa Mwenyezi Mungu unaendelea kwa mawasii kumi na wawili toka kizazi chake. Kizazi ambacho Mwenyezi Mungu alikitakasa na kukiondolea uchafu nao ni Maimam wema waongozaji upande wa haki na makhalifa wema ambao Mtume (s.a.w.w.) aliwaacha pamoja na Qur’ani tukufu. Akauambia umma wake ushikamane navyo pamoja ili wapate mafanikio na wema hapa duniani na kesho Akhera. Imam Ali bin Abu Talib (a.s.) ndiye Imam wa kwanza kati ya Maimam vion- gozi wema na kati ya makhalifa wa Mwenyezi Mungu na watawala Wake katika ardhi Wake.
Mtume (s.a.w.w.) alitoa maelezo juu ya uimamu wake,1 hiyo ni baada ya kumlea yeye mwenyewe na kumpandikiza elimu yake, sifa zake nzuri na maadili yake mazuri. Akafahamika kwa kufuata haki, jihadi yake, kujitolea kwake, kumwabudu Mwenyezi Mungu na kupenda kuhami ujumbe wa Mola Wake. Hivyo akamkabidhi jukumu baada ya kuubainishia umma jinsi yeye anavyostahiki na kufaa cheo hiki cha uwasii na uongozi. Alibainisha hayo tangu mwanzo wa utume wake uliobarikiwa.
Imam Ali aliwatangulia maswahaba wote katika kuukubali ujumbe wa Mwenyezi Mungu huku akiwatangulia ndugu wote wa karibu wa Mtume (s.a.w.w.) katika kumsaidia Mtume (s.a.w.w.).2Akamhami katika kipindi chote cha zama za Makka.3 Akalala kitandani kwa Mtume (s.a.w.w.) usiku wa kuhama4huku akifidia nafsi yake dhidi ya nafsi ya Mtume (s.a.w.w.). Aliendelea kuuhami Uislamu kipindi chote cha miaka yote ya matatizo5 huku akitii amri za Mtume katika kila jambo na kila sehemu.
Kukua Kwa Imam Ali Bin Abu Talib Na Hatua Za Maisha Yake
Nasaba Yake Ing’aayo
Imam Ali (a.s.) ametokana na kuzaliwa na wazazi wawili watukufu watakasifu ambao hawajachafuliwa na shirki wala uchafu wa kijahiliya. Imam Ali (a.s.) amesema:
“Naapa kwa Mwenyezi Mungu baba yangu wala babu yangu Abdul Muttalib wala Hashim wala Abdul Manafi katu hawakuabudu sanamu……. Walikuwa wakiswali wakielekea Al-Kaaba kwa kufuata dini ya Ibrahim huku wakishika- mana nayo.6Hivyo baba ni Abu Talib na jina lake ni Abdu Manafi. Babu ni Abdul Mutalib na jina lake ni Shaybatul-hamdi.
Babu wa baba yake ni Hashim na jina lake ni Amru mtoto wa Abdu Manafi na jina lake ni Al-Mughira mtoto wa Quswayyi mtoto wa Kilabi mtoto wa Murrat mtoto wa Luayyi mtoto wa Ghalib mtoto wa Fahri mtoto wa Malik mtoto wa An-Nadhar mtoto wa Kinanat mtoto wa Khuzaymat mtoto wa Mudrikat, mtoto wa Iliyasa, mtoto wa Mudhar, mtoto wa Nazar, mtoto wa Maaddi, mtoto wa Adinan. Adinan ana- tokana na Ismail mtoto wa Ibrahim kipenzi cha Mwenyezi Mungu.”
Abu Talib ni mdogo wa Abdullah mzazi wa Mtume (s.a.w.w.) kwa baba na mama. Alimlea Mtume (s.a.w.w.) utotoni mwake huku akimnusuru ukubwani, akamtetea na kumlinda huku akivumilia maudhi toka kwa mushrikina wa kiquraishi huku akimlinda dhidi yao. Hivyo kwa ajili yake akapatwa na matatizo makubwa huku akikumbana na misukosuko mikali lakini akavumilia katika kumnusuru na kusimamisha jambo lake mpaka maquraishi wakakata tamaa dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) kwani walikuwa wameshindwa mpaka alipofariki Abu Talib.
Hakuamrishwa kuhama isipokuwa baada ya kufariki Abu Talib. Abu Talib alikuwa muislamu asiyedhihirisha Uislamu wake, kwani laiti angekuwa akidhihirisha basi asingeweza kumnusuru Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) kikamilifu kama alivyomnusuru.
Zaidi ya hapo ni kuwa Abu Talib alikubali usahihi wa unabii wa Mtume (s.a.w.w.) mara nyingi katika mashairi yake mfano kauli yake: “Ukanilingania nami nikajua kuwa wewe ni mkweli. Umesema kweli na kabla ya hapo ulikuwa mwaminifu. Nilijua kuwa dini ya Muhammad ni dini bora kati ya dini zote za mwanadamu”.7
Mama yake ni Fatima binti Asad bin Hashim bin Abdul Manafi bin Quswayyi.Yeye ndiye binti wa kwanza toka familia ya Hahim aliyezaa na kijana wa familia ya Hashim. Imam Ali (a.s.) alikuwa ndiye mtoto wake mdogo kati ya watoto wake ambao ni Jafar, Aqil na Talib. Mama yake aliukubali Uislamu baada ya watu kumi wa mwanzo.
Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akimkirimu na kumtukuza huku akimwita: Mama yangu. Na alipokaribiwa na umauti alimuusia Mtume (s.a.w.w.) na Mtume akakubali usia wake na hivyo akamsalia na kumshusha ndani ya mwanandani na kumlaza humo, hayo ni baada ya kumvisha kanzu yake (ya Mtume). Hapo maswahaba zake wakamwambia:
“Hatujaona ukifanya kwa yeyote mfano wa uliyofanya kwake.” Akajibu: “Hakuna mtu aliyekuwa mwema kwangu baada ya Abu Talib zaidi yake. Hakika nimemvisha kanzu yangu ili avishwe mapambo ya peponi, na nimemlaza na kanzu hiyo ili uzito wa kaburi uwe mwepesi kwake.”8
Al-Mufid na At-Tabariy wameongeza kuwa: “Mtume (s.a.w.w.) alimtamkisha akiri utawala wa mwanae Ali (a.s.). Riwaya hiyo ni maarufu.9 Na yeye ndiye mwanamke wa kwanza aliyetoa kiapo cha utii kwa Mtume wa Mwenyezi Mumgu (s.a.w.w.) kati ya wanawake wote.10
Kuzaliwa Kwake Kulikobarikiwa
Mashuhuri ni kuwa alizaliwa Makka ndani ya Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu (Al-Kaaba), siku ya Ijumaa, siku ya kumi na tatu ya mfungo kumi (Rajab) mwaka wa thelathini tangu kutokea kwa tukio la mwaka wa tembo.11
Al-Hakim An-Nisabury amesema: “Zimeenea habari kuwa Fatima binti Asad alimzaa kiongozi wa waumini Ali bin Abu Talib ndani ya Al-Kaaba.”12
Al-Mufid na wenzake wamesema: “Hakuzaliwa yeyote yule ndani ya Al-Kaaba kabla yake wala baada yake. Mwenyezi Mungu alifanya hivyo kwa ajili ya kumpa heshima na kutukuza nafasi yake.”13
Mama wa Ammarat binti Ubadat amesema: “Abu Talib alimshika mkono Fatima binti Asad akaenda naye Kaaba kisha akamwambia: “Kaa kwa jina la Mwenyezi Mungu,” hapo akapatwa na uchungu kisha akajifungua kijana mwenye furaha msafi aliyesafika ambaye sijamwona mwingine kwa uzuri wa uso wake. Hapo akamwita jina, Ali, na Mtume (s.a.w.w.) akambeba mpaka nyumbani kwa Fatima.14
Kupewa Jina Na Lakabu Zake
Ibnu Abul-Hadid na wenzake wamesema: “Hakika jina lake la kwanza aliloitwa na mama yake ni Haydar (Simba) likiwa ni jina la babu yake, yaani baba wa mama yake Asad (Simba) bin Hashim. Ndipo baba yake akambadili jina na kumwita Ali.”15
Mtume (s.a.w.w.) akampa kuniya ya Abu-Turab, hiyo ni baada ya kumuona yuko katika hali ya sijida huku uso wake umo ndani ya udongo. Jina hili ndilo alilolipenda sana yeye mwenyewe.16
Mwanawe Hasan (a.s.) wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akimwita baba Husain. Huku mwanae Husain akimwita baba Hasan. Pia aliitwa baba wa wajukuu wawili na baba wa manukato mawili. Mtume alimpa lakabu ya: Kiongozi wa waumini (Amirul-Mu’minin), huku muhajirina na ansari wakimwita kwa lakabu hiyo.17
Pia alipewa lakabu ya Mteule {Al-Murtadha}, walii wa Mwenyezi Mungu, kipenzi cha Mwenyezi Mungu, wasii wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Simba wa Mwenyezi Mungu, upanga wa Mwenyezi Mungu, ndugu wa Mtume, bwana wa waarabu, kijana wa kiquraishi, mgawa pepo na moto, Lango wa Jiji la Elimu, bwana wa waislam, jemedari wa waumini, kiongozi wa kundi mashuhuri, Imam wa wachamungu na mkweli mno.
Baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.) lakabu yake mashuhuri ilikuwa ni wasii.18 Lakabu hii ilikuwa mashuhuri kwake tangu mwanzo, hivyo ikaenea sana mpaka ikachukua nafasi ndani ya vitabu vya lugha mfano: Lisanul-Arab, Tajul-Urus na vinginevyo. Wasomi (Baadhi) wa kisunni walijitahidi sana kutaka kuficha habari za uwasii wake na kutaka kuleta tafsiri nyingine kinyume na ile iliyoenea.19
Malezi Na Makuzi Yake
Haraka sana Mtume (s.a.w.w.) alimtilia umuhimu maalumu Imam Ali bin Abu Talib (a.s.), alimpenda sana na kumwambia mama yake: “Weka kitanda chake karibu na kitanda changu.” Mtume alikuwa akitawala sana malezi yake, hivyo alikuwa akimtoharisha Ali wakati wa kuogeshwa na akimuwekea maziwa mdomoni wakati wa kunywa maziwa.
Alichezesha kitanda chake wakati wa kulala huku akimbembeleza awapo macho. Akimbeba kifuani kwake na shingoni huku akisema: “Huyu ni ndugu yangu, walii wangu, mwenye kuninusuru, mteule wangu, tegemeo langu, kinga yangu, mkwe wangu, wasii wangu, mme wa binti yangu, wasii wangu na khalifa wangu mwaminifu”. Daima alikuwa akimbeba na kuzunguka nae katika milima na mabonde ya Makka.20
Imam Ali (a.s.) yeye mwenyewe amefafanua makuzi yake ya mfano ambayo yamejaa heshima kwa kiwango cha juu, akasema katika hotuba yake kuwa: “Mnajua nafasi yangu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ukaribu wa karibu na nafasi mahsusi niliyonayo kwake. Alinilea nikiwa mtoto akinikumbatia kifuani mwake na kitandani kwake. Akinigusisha mwili wake, akininusisha harufu yake. Alikuwa akitafuna kitu kisha akinilisha, hakupata uongo wa kauli yoyote toka kwangu, wala kosa lolote la kitendo.
Nilikuwa nikimfuata kama mtoto aliyeachishwa ziwa amfatavyo mama yake, huku kila siku akiniinua juu kwa kuniongezea sehemu ya maadili yake huku akiniamrisha kumfuata. Kila mwaka alikuwa akienda pango la Hira hakuna anayemuona isipokuwa mimi tu. Wala hakuna nyumba hata moja kipindi hicho iliyokuwa imekusanya waislam wasiyokuwa Mtume, Khadija na mimi nikiwa watatu wao, nikiona nuru ya wahyi na utume huku nikinusa harufu ya unabii. Nilisikia mlio wa shetani pindi wahyi ulipomshukia Mtume, nikase- ma: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni sauti ya nini hii?” Akajibu: “Huyu ni shetani amekata tamaa dhidi ya kuabudiwa, hakika wewe unasikia ninayosikia na unaona nionayo isipokuwa wewe si nabii lakini wewe ni waziri na hakika wewe upo juu ya heri.”21
Hatua Za Maisha Yake
Kuanzia alipozaliwa mpaka Mtume (s.a.w.w.) alipopewa utume, nacho ni kipindi cha miaka kumi. Kisha kipindi cha miaka kumi kuanzia alipopewa Mtume (s.a.w.w.) utume mpaka alipohama. Kisha kipindi cha miaka kumi mpaka alipofariki Mtume (s.a.w.w.). Kisha miaka ishirini na tano mpaka kumalizika utawala wa Uthmani. Kisha miaka mitano ambayo ndio muda wa serikali yake.
Muhtasari
Ali bin Abu Talib (a.s.) alitokana na asili ile ile aliyotokana nayo Mtume (s.a.w.w.) hivyo nasaba yake na nasaba ya Mtume (s.a.w.w.) ni moja.
Ali (a.s.) alitofautiana na maswahaba wengine kwani hakuna shirki yoyote iliyomuingia. Kisha akawa ni mtu mahsusi kwa Mtume (s.a.w.w.) hivyo akawa akimfunza mafunzo yatokanayo na hekima za Mwenyezi Mungu na elimu ya Mola Wake, jambo ambalo hakulipata swahaba mwingine yeyote.
Ali (a.s.) alidhihirisha utiifu na ufuataji kamilifu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.), akajipamba kwa maadili mazuri, akajitolea nafsi na kila lenye thamani kwa ajili ya itikadi ya Uislamu.
Mwenyezi Mungu alimteua awe wasii wa Mtume Wake (s.a.w.w.) hivyo akasimamia jukumu la uwasii kwa ukamilifu mpaka adui akakiri hilo kabla ya rafiki.
Imam Ali (a.s.) alibeba majina na lakabu nzuri ambazo zinaonyesha jinsi alivyoshikamana sana na Mwenyezi Mungu na alivyokuwa na itikadi salama ya Mwenyezi Mungu na maadili bora mazuri.
Maswali
1. Ni jukumu gani ambalo Mtume (s.a.w.w.) alimpa Imam Ali (a.s.) baada yake? 2. Ni kitu gani kinachomtofautisha Imam Ali (a.s.) na maswahaba wengine wa Mtume (s.a.w.w.)? 3. Elezea jinsi gani Imam Ali (a.s.) alivyokuwa Khalifa wa Mtume (s.a.w.w.) na wala si mwingine? 4. Ni uhusiano gani wa kinasaba uliyopo kati ya Mtume Muhammad na Imamu Ali? 5. Ni karama zipi ambazo Mwenyezi Mungu alimfadhilisha kwazo Imam Ali (a.s.) wakati wa kuzaliwa kwake? Andika riwaya na yote unayoweza kuyapata ndani ya riwaya hiyo. 6. Kwa nini jina la Abu Turab ndilo alilolipenda sana Imam Ali? 7. Imam Ali (a.s.) aliishi na Mtume (s.a.w.w.) miaka mingapi?
· 1.Al-Muraj’ati cha Sayyid Abdul-Husayn Sharafudin, namba 20 na 68.
· 2.Taarikh Tabariy, Juz. 2, Uk. 403. Ihqaqul-Haqi, Juz. 4 Uk. 58-70. Shawahidut-Tanziil, Juz. 1, Uk. 420.
· 3.Al-Manaqib cha Shahru Ashuub, Juz. 2, Uk. 65. Aayanus-Shia, Juz. 1, Uk. 372.
· 4.Al-Mustadraku alas-Sahihayni, Juz. 3, Uk. 4. Biharul-An’war, Juz. 19, Uk. 28.
· 5.Imam Ali alishiriki vita vyote kasoro vita vya Tabuk, kwa mfano tu rejea kitabu Al-Manaqib, Juz. 2, Uk. 81. Qadatuna, Juz. 2, Uk. 78-148.
· 6.Tazama Imam Abu Talib cha Fakhar bin Muidu Al-Musawiy. Al-Ghadiri ya Amini, Juz. 7, Uk. 330.
· 7.Aayanus-Shia, Juz. 1, Uk. 324.
· 8.Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz. 1, Uk. 13-14.
· 9.Al-Ir’shadi, Juz. 1, Uk. 5. Iilamul-Waraa, Juz. 1, Uk. 306.
· 10.Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz. 1, Uk. 13-14.
· 11.Al-Ir’shadi, Juz. 1, Uk. 5.
· 12.Al-Mustadrak alas-Sahihayn, Juz. 3, Uk. 483.
· 13.Al-Ir’shadi, Juz. 1, Uk. 5. Al-Fusulul-Muhimmah, Uk. 30.
· 14.Kashful-Ghummah, Juz. 1, Uk. 59 na 60.
· 15.Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz. 1, Uk. 12. Kashful-Ghummah, Juz. 1, Uk. 61.
· 16.Iilamul-Waraa, Juz. 1, Uk. 307. Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz. 1, Uk 11.
· 17.Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz. 1, Uk. 12, 13, 143.
· 18.Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz. 1, Uk. 12, 13, 143.
· 19.Tazama kitabu Maalim Madrasatayn, Juz. 1 Uk. 295 – 340, chapa ya tano.
· 20.Kashful-Ghummah, Juz.1, Uk. 60.
· 21.Nahjul-Balaghah, hotuba ya 192.