Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
QURAN

Surat Yunus 15-18

2016/01/19

Surat Yunus 15-18

Surat Yunus 15-18

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 309 tunayoianza kwa aya ya 15 ambayo inasema:

"Na wanaposomewa aya zetu zilizo wazi, wale wasiotaraji kukutana nasi husema: Lete quran isiyokuwa hii au ibadilishe. Sema: Siwezi kuibadilisha kwa hiyari ya nafsi yangu. Mimi sifuati ila ninayofunuliwa kwa Wahyi. Hakika mimi naogopa nikumuasi Mola wangu adhabu ya siku iliyo kuu."

Washirikina na waabudu masanamu ambao walikuwa walinganiwa wa wito wa tauhidi aliokuja nao Bwana Mtume Muhammad (s), badala ya kuachana na itikadi na ibada zao hizo potofu, ni wao ndio waliomtaka bwana Mtume (s) akidhi matakwa yao kwa kuzifuta katika Quran zile aya zinazokataza na kukemea ibada ya masanamu, au hata ikiwezekana kuleta kitabu kingine kabisa kisicho na aya za aina hiyo, ili hapo ndipo wao wamwamini Mtume huyo wa Allah. Hali ya kuwa lengo la Mitume ni kuwaelekeza watu kwenye uongofu na si kutaka kujipatia wafuasi wengi zaidi. Kwa maana kwamba katu hawawezi kukubali matakwa yasiyo ya kimantiki ya watu kwa sababu tu ya kutaka kupata idadi kubwa zaidi ya wafuasi. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa hakuna mtu yeyote yule hata Mtume aliye na haki ya kuibadilisha hata aya moja ya vitabu vya mbinguni vilivyoteremshwa na Allah, bali manabii hao, wao wenyewe ni wenye kujisalimisha na kutii kikamilifu kila kilichokuja katika risala ya wahyi walioteremshiwa na Mola wao. Aidha aya inatuelimisha kuwa msingi wa mafundisho ya Uislamu ni kushikamana nayo kama yalivyo yale yaliyoletwa na Mwenyezi Mungu, na wala hakuna thamani yoyote kuifanya dini iwe na wafuasi wengi zaidi kwa gharama ya kubadilisha na kupotosha mafundisho yake ya asili.

Zifuatazo sasa ni aya za 16 na 17 ambazo zinasema:

"Sema: Mwenyezi Mungu angeli taka nisingeli kusomeeni, wala nisingeli kujuvyeni. Kwani nilikwisha kaa nanyi umri mzima kabla yake! Basi, je hamzingatii?" "Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia uwongo Mwenyezi Mungu na akazikanusha aya zake? Hakika hawafaulu wale wafanyao maovu."

Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinaendelea kutoa jibu kwa wale watu waliomtaka Bwana Mtume Muhammad (s) aibadilishe quran na kuwaambia, Mtume huyu ameishi na nyinyi kwa miaka arubaini. Lau quran hii ingekuwa imetokana na fikra zake yeye mwenyewe bila shaka katika kipindi hicho chote mungeweza kushuhudia maneno mithili ya hayo katika fikra zake. Isitoshe ni kuwa yeye Muhammad (s) hakuwahi kusoma popote wala kufunzwa na yeyote hata mseme labda hii quran itakuwa ni matunda ya elimu hiyo aliyokuwa amejifunza hapo kabla. Hivyo wale wanomtaka yeye aibadilishe quran hakika wanachofanya ni kuzikadhibisha aya za Mwenyezi Mungu na kumzulia uwongo yeye Mola Muumba, jambo ambalo ni sawa na kumfanyia dhulma kubwa kabisa yeye Mola, Mtume wake na kitabu chake cha quran. Baadhi ya tunayojifunza katika ya hizi ni kuwa vitabu vya mbinguni ni wahyi utokao moja kwa moja kwa Allah na wala si kitu kinachotokana na fikra za Mitume au mtu mwengine yoyote. Aidha zinatutaka tuelewe kuwa dhulma kubwa kabisa ni ile ya kupotosha na kuyabadilisha mafundisho asili ya dini.

Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 18 ambayo inasema:

"Nao wanaabudu (waungu) wasiokuwa Mwenyezi Mungu wasioweza kuwadhuru wala kuwanufaisha. Na wanasema: "Hao ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu". Sema:"Je Mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi?".Ameepukana na upungufu (wa kutaka mshirika), na ametukuka na hao wanaowashirikisha naye."

Washirikina walikuwa wakiyaabudu masanamu ambayo si kwamba yalikuwa yana uwezo wa kuwadhuru hata kwa kukhofia hilo walihisi kuwa hawana budi ila kuwaabudu, na si kwamba pia kuna faida walikuwa wakipata kwa masanamu hayo hata tamaa ya kupata faida hiyo iwe sababu ya kuwafanya wawapigie magoti na kuwaomba. Ama hoja waliyokuwa wakiitoa washirikina hao ni kuwa masanamu hayo yalikuwa ni wasita na kiunganishi kati yao na Mwenyezi Mungu. Hata hivyo hoja hii haikubaliki kwa sababu Mwenyezi Mungu hakuyafanya masanamu hayo ni wasita, kiunganishi na waombezi wa waja wake kwake yeye. Hii ni tofauti na wala haiwezi kulinganishwa na suala la tawasul wanayofanya watu kwa Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu na kuomba wawatakie shufaa mbele ya Mola, kwani hao wako katika maisha maalumu ya barzakhi waliyojaaliwa na Allah na vile vile ni yeye Mola mwenyewe aliyewaelekeza watu watumie wasita wa waja wake hao walio wateule kwa ajili ya kumfikia yeye. Funzo moja muhimu tunalolipata kutokana na aya hii ni kuwa tujihadhari na kukifanya kitu au mtu yeyote yule kuwa mshirika wa Allah katika uungu, au kukifanya kitu au mtu kuwa na hadhi ya kuweza kutushufaia na kutuombea mbele ya yeye Mola, ghairi ya wale yeye Allah mwenyewe aliowapa daraja hiyo ya kuwa waombezi kwa waja wake.

Darsa ya 309 imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na kila aina ya shirki. Amin.