Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
QURAN

Surat Yunus 11-14

2016/01/19

Surat Yunus 11-14

Surat Yunus 11-14

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii. Sura ya 10 inayoitwa Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hapa tunaianza kwa aya ya 11 ambayo inasema:

"Na lau kama Mwenyezi Mungu angeliwafanyia watu haraka kuwaletea shari, kama wanavyojihimizia kuletewa kheri, bila shaka wangelisha timiziwa ajali yao. Lakini tunawaacha wale wasiotumainia kukutana nasi, wakihangaika katika upotovu wao."

Moja ya utaratibu ambao Allah sw ameuweka kuhusiana na waja wake ni kutoa muhula na fursa kwao, ili kila mmoja aamue na kuchagua kwa hiyari yake njia gani anayotaka kufuata, ikiwa ni ya kuiamini haki au kuikufuru. Kwa bahati mbaya idadi kubwa ya watu huwa hawaitumii kwa njia sahihi fursa hiyo adhimu wanayotunukiwa na Mola wao, na badala yake huogelea kwenye dimbwi la maasi na maovu. Pamoja na hayo Mola aliye mrehemevu huendelea kuamiliana kwa upole na ukarimu na waja wake kwa kuwapa fursa nyingine ya kutubia kwa madhambi waliyoyafanya ili wapate maghufira na msamaha wake. Ama ikiwa hata baada ya kupata fursa hiyo mja ataamua kuselelea katika kutenda maovu na kumwasi Mola Muumba, mja wa aina hiyo huachwa kama alivyo aendelee kufuata njia hiyo ya upotofu hadi kipindi cha uhai wake kinapomalizika, ambapo hapo huelekea ulimwengu mwingine wa akhera na huko hupata jaza na malipo ya maovu na maasi aliyoyafanya hapa duniani.

Aya hii pamoja na mambo mengine inatufunza kuwa kutoangamizwa kwa makafiri na madhalimu hapa duniani hakumaanishi kuwa yale wayafanyao ni ya sawa au kwamba Mwenyezi Mungu sw anashindwa kuwateremshia adhabu. Bali hiyo inatokana na ile fursa na muhula ambao Allah ameamua kuwapa waja wake hao.

Ifuatayo sasa ni aya ya 12 ambayo inasema:

"Na mtu akiguswa na shida hutuomba, naye kaegesha ubavu, au kakaa, au kasimama. Lakini tukimwondoshea shida yake huendelea kama kwamba hakupata kutuomba tumwondoshee shida iliyompata. Namna hivi wamepambiwa warukao mipaka yale waliyokuwa wakiyatenda."

Raha na neema za kidunia wapenzi wassomaji humfanya mtu aghafilike na Mola wake na kuikumbatia dunia. Ama shida, masaibu na matatizo mara nyingi humfumbua macho mtu huyo na kumfanya aelewe kuwa binadamu ni kiumbe dhaifu kiasi kwamba pale anapotingwa na matatizo hutambua jinsi ya kumwomba na kumlingana Mwenyezi Mungu kutaka msaada, awe kitandani anaugua maradhi akiomba aponywe, au baharini na angani pale mauti yanapomkabili akawa hana njia nyingine yoyote ya kujiokoa, na hivyo kutaka nusra ya Mwenyezi Mungu sw. Ya laiti baada ya mja kuitikiwa kilio chake hicho angeweza walau kumshukuru tu Mola wake na kuendelea kumkumbuka japo kwa siku chache. Lakini wapi! Akthari ya watu humsahau haraka Mwenyezi Mungu kana kwamba hawakuwa wametingwa na masaibu na ni yeye Mola aliyetukuka ndiye aliyewaondolea masaibu hayo. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa imani ya kuwepo na Mungu mmoja imekita ndani ya nafsi ya kila mwanadamu, na kwa kweli maafa, shida na misukosuko huwa ndiyo chachu ya kuiamsha fitra na maumbile hayo yaliyolala ya kukiri kuweo kwa yule aliye na uwezo mutlaki wa kila kitu.

Aya za 13 na 14 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

"Na kwa yakini tumekwisha ziangamiza uma nyingi kabla yenu walipodhulumu, na waliwajia Mitume wao kwa hoja zilizowazi; lakini hawakuwa wenye kuamini. Namna hivi tunawalipa watu wanaofanya waovu." "Kisha tukakufanyeni nyinyi ndio wenye kushika mahala pao baada yao katika ardhi ili tuone jinsi mtakavyotenda."

Ijapokuwa kama tulivyotangulia kunena katika aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu huwapa muhula wale wanaomwasi na kufanya madhambi na kutowaangamiza papa hapa duniani, lakini hili huwa ni tofauti linapohusu umma au kaumu nzima ya watu, pale watu hao wanapokithirisha dhulma na madhambi, kwani hatima ya kaumu za aina hiyo ni kuangamizwa. Kisha baada ya kuangamizwa kaumu hizo huletwa mahala pao kaumu ya watu wengine ambao wanatakiwa kuyachukulia yale yaliyowasibu waliowatangulia kuwa ni ibra na funzo kwao, vinginevyo na wao pia watapatwa na majaaliwa kama yao. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa dhulma na uonevu ni mambo yanayoandaa mazingira ya kuangamizwa watu, tabaan wale watu ambao hakuna matumaini tena kwa wao kuamini na kuifuata haki. Halikadhalika aya zinatuelimisha kuwa hatima na majaaliwa ya watu yako mikononi mwao wenyewe, na kwa kweli ni matendo yao mabaya na maovu ndiyo yanayoainisha wawe na hatima gani. Na pia aya zinatufunza kwamba endapo mtu atajiona amepata madaraka au mamlaka ya utawala, ajue kuwa huo ni mtihani ambao Mwenyezi Mungu amempa kumjaribu. Tunamwomba Allah atuwafikishe kufuzu mitihani yake na atuzindue kila pale tunapoghafilika na kumkumbuka yeye. Amin.