Bi-Khadijah-a.s
Sura Ya Pili: Maisha ya Mwanzo ya Khadija -tul-Kubra (R)
Khadija alizaliwa Makka. Alikuwa mtoto wa kike wa Khuwaylid bin Asad bin Abdul Uzza bin Qusayy. Qusayy alikuwa babu aliyejulikana sana kwenye ukoo wa Khadija vile vile kwenye ukoo wa Muhammad Mustafa, wa uzao wa Bani Hashim, aliyekuja kuwa Mtume wa Uislamu (S.a.w.). Kwa hiyo Khadija alitokana na nasaba yenye asili moja na Bani Hashim. Baada ya Bani Hashim, familia yake ilikuwa tukufu na yenye kuheshimika sana Arabuni pote. Familia ya Khadija haikuwa mashuhuri kwa utajiri tu bali pia kwa ubora wa tabia yake.
Khuwaylid, baba wa Khadija pia alikuwa mfanyabiashara kama wenzake wengine wengi wa kabila la Quraysh wa Makka. Kama walivyokuwa wafanyabiashara wa kabila la Qurayshi wengi, baba yake Khadija naye alipata mafanikio ya utajiri kutokana na biashara ya nje. Wafanyabiashara wa Makka walituma misafara miwili kila mwaka mmoja wakati wa kiangazi ambao ulikwenda Syria na mwengine wakati wa kipupwe ambao ulipelekwa Yemen.
Misafara hii ya kibiashara ilibeba mazao ya jangwani na bidhaa zilizo tengenezwa Makka na sehemu za jirani yake na ziliuzwa kwenye masoko ya Syria na Yemen. Aidha waliuza farasi-chotara Syria. Aina hii ya farasi ilithaminiwa sana Syria na nchi jirani. Baada ya kuuza bidhaa zao na farasi-chotara wao, wafanyabiashara hao walileta nafaka, mafuta ya zeituni, matunda, kahawa, nguo, bidhaa za anasa na vitu vingine vilivyotengenezwa kwa ajili ya kuviuza Makka. Hivyo walipata faida Syria, Yemen na Makka.
(Biashara hii ya Makka imetajwa kwenye Quran Majid, Sura ya 106)
Biashara ya nje ilikuwa ndio msingi mkubwa wa uchumi wa Makka. Makka ilikuwa haina ardhi ya kilimo wala maji ya kilimo cha umwagiliaji. Watu wa Makka, katika hali hiyo, hawakuweza kulima mazao ya chakula. Walitegemea biashara baina yao na Syria na Yemen ili wajilishe. Kutokana na faida waliyopata walinunua nafaka na vitu vingine muhimu katika maisha.
Kila msafara ulikuwa na kiongozi. Kiongozi huyu alitakiwa kuwa mtu mwenye sifa zisizo za kawaida. Usalama na kufaulu kwa msafara katika biashara ya mauzo na manunuzi, ilitegemea sana maamuzi ya kiongozi. Kiongozi alikuwa na kazi ya kulinda msafara usishambuliwe na wanyang\'anyi na mabedui wa jangwani. Kiongozi aliweza kufanya kazi hii kwa kuandikisha wapiganaji kutoka makabila mbalimbali na kuunda vikosi kufuatana na ukubwa wa msafara. Vikosi vilisindikiza misafara mpaka mwisho wa safari. Misafara yote iliyokwenda masafa marefu, ilikuwa chini ya ulinzi wa kijeshi.
Kiongozi wa msafara pia alitakiwa kuwa na kipaji cha pekee kwa kumuongoza kwenye jangwa lisilo na njia wakati wa mchana, na alitakiwa kuwa na uwezo wa kutambua njia ya msafara wakati wa usiku. Kiongozi alitakiwa kuwa na ujuzi wa kuzitumia nyota katika safari wakati wa usiku. Alikuwa anatakiwa kuhakikisha kuwepo kwa maji wakati wa safari ndefu ya kwenda Syria au kwenda Yemen. Alitakiwa kuchukuwa tahadhari dhidi ya majanga yasiyotegemewa kama vile kimbunga cha mchanga na msongamano wa miale ya taa za misafara. Alikuwa anatakiwa kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya kwanza ya tiba endapo msafiri aliugua au aliumia.
Kwa ujumla, kiongozi alitakiwa kuwa na uwezo wa kushughulikia dharura yoyote ile. Wafanyabishara wa Makka, walimteua kiongozi wa misafara yao baada ya kuchunguza historia yake kwa uangalifu sana. Jopo la wasafiri wazoefu lilipitia majina ya watu waliopendekezwa kwa kazi hiyo.
Jopo la wachunguzi halikuridhishwa na sifa yoyote iliyo chini ya kiwango cha uwezo wa kiongozi wa msafara kuongoza kwa ustadi kwenye njia zisizo na michoro kwenye "bahari" ya mchanga, na kufaulu kwake kurudisha misafara ya "meli za jangwa" yaani ngamia pamoja na mizigo yao nyumbani salama. Ili akubalike kwa jopo, mtahiniwa alitakiwa kuonyesha kwamba alikuwa na uzoefu wa kutosha sana kuhusu utaratibu wa usafirishaji wa misafara ya biashara na "vitambulisho" vyake vilitakiwa awe hana kosa.
Mama yake Khadija alikufa mnamo mwaka wa 575 A.D.,na Khuwayled baba yake, alikufa mnamo mwaka wa 585 A.D. Baada ya kifo cha Khuwayled, watoto wake walirithi utajiri wake na waligawana mali hiyo. Utajiri una hatari zake. Utajiri unaweza kumfanya mtu akaishi maisha ya kubweteka na anasa. Khadija alitambua tabia ya utajiri kwa undani, na aliamua kutoruhusu utajiri kumfanya yeye asifanye kazi.
Khadija alikuwa na akili ya kiwango kisicho cha kawaida na uwezo wa tabia ya kuishinda changamoto ya utajiri, na aliamua kujenga himaya ya urithi kutoka kwa baba yake. Alikuwa na ndugu wengi lakini miongoni mwa wote hao, ni yeye peke yake ndiye aliyerithi uwezo wa baba yao kuwa tajiri. Lakini alionyesha katika kipindi kifupi sana kwamba hata kama hangekuwa amerithi utajiri wa baba yake, bado angeweza kupata utajiri kwa bidii yake mwenyewe.
Baada ya kifo cha Khuwayled, Khadija alichukuwa kazi ya kusimamia biashara ya familia na aliipanua haraka sana. Faida aliyoipata aliwasaidia fukara, wajane, watoto yatima, wagonjwa na wasiojiweza.
Endapo palikuwepo na wasichana fukara, Khadija aliwasaidia waolewe na aliwapa mahari.
Mmoja wa wajomba zake alijitolea kumsaidia kama mshauri wake katika kuendesha biashara, na ndugu zake wengine katika familia pia walimsaidia katika biashara wakati wowote alipohitaji msaada wao. Lakini hakumtegemea mtu yeyote katika kufanya uamuzi. Khadija alitegemea zaidi uamuzi wake mwenyewe ingawaje alikubali kushauriwa na kufikiria namna ya kuutumia ushauri huo. Ndugu wakubwa katika familia walitambua kwamba alikuwa hapendi ubia.
Wafanya biashara wengi waliokuwa na mizigo ya kuuza Syria au Yemeni, walisafiri na misafara yao wenyewe na kushugulikia mauzo yao binafsi. Lakini wakati mwingine mfanyabiashara alishindwa kuondoka Makka. Katika hali kama hiyo mfanyabiashara huyo alimkodi mtu kwenda na msafara badala yake. Mtu aliyeteuliwa kwa madhumuni haya, alitakiwa awe na tabia njema kwa uaminifu wake na uwezo wa kufanya biashara. Mtu wa namna hii aliitwa Wakala au Meneja.
Khadija alikuwa mtu wa nyumbani pia ndugu zake na binamu zake hawakupenda kusafiri na misafara. Kwa hiyo, alimuajiri wakala wakati wowote msafara ulipotoka kwenda nje (ya Hijazi), na kumfanya wakala huyo kuwa na madaraka ya kupeleka bidhaa zake kwenye masoko ya nje kuziuza huko.
Kwa uwezo mzuri wa kuteua mawakala, na kununua na kuuza wakati na mahali muafaka aliweza kupata faida kubwa sana, na baadaye, akawa mfanyabiashara tajiri sana wa Makka. Ibn Sa\'ad anasema kwenye Tabqaat yake kwamba misafara ya wafanya biashara wa Makka ilipoanza safari, mzigo wa Khadija peke yake ulikuwa sawa na mizigo ya wafanyabishara wengine wote wa Qurayish katika msafara huo.
Alikuwa dhahiri kwa kila mtu ni kama msemo "golden touch" ("mguso wa dhahabu") yaani kila atakacho kigusa hata kama ni vumbi litageuka kuwa dhahabu. Watu wa Makka, katika hali hiyo, walimpa jina la Malkia wa Qurayish. Aidha walimwita Malikia wa Makka.
Wakati huo Bara Arabu ilikuwa jamii ya kipagani, na Waarabu waliabudu masanamu mengi na miungu masanamu, ambao waliamini walikuwa na uwezo wa kuleta bahati njema kwao. Lakini ibada yao ya kuabudu masanamu haikuwa adilifu na ilikuwa ibada ya kishenzi, tabia, mila zao na adabu zilikuwa za kukatisha tamaa.
Ulevi ulikuwa mojawapo wa uovu wao, na walikuwa wacheza kamari wasiokanyika. Walikuwa wanagaagaa kwenye shimo la dhambi na ujinga. Qur\'an Majid inasadikisha hali yao kwenye Aya ifuatayo:
هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِنْ كَانُوا مِنْ قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {2}
"Yeye ndiye aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase na awafunze Kitabu na Hekima, ijapokua kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhahiri" (Qur\'an 62:2).
Lakini si kwamba nchi ilikuwa haina watu ambao waliona ibada ya masanamu kuwa ya kuchukiza. Watu hawa ambao walikuwa wachache sana kwa idadi waliitwa "Mahanifi" ("Hanifs") yaani wanaume na wanawake "ambao waliasi ibada ya kuabudu masanamu." Makka nayo ilikuwa na watu hao wachache kwa idadi "Mahanifi" na baadhi yao walikuwa kwenye ukoo wa Khadija. Mmoja wao alikuwa binamu yake wa kwanza, Waraqa bin Naufal.
Waraqa alikuwa mkubwa katika ndugu zake wote, na nywele zake zote zilikwisha kuwa rangi ya jivu. Aliwashutumu Waarabu kwa kuabudu masanamu na kwa kuacha njia ya kweli ya mababu zao - Mitume Ibrahim na Ismaili. Ibrahim na Ismaili walifundisha somo la Tauhiid -Imani ya Kumpwekesha Muumba. Lakini Waarabu walisahau somo hilo, na wakaingia kwenye shiriki. Waraqa aliwadharau Waarabu kwa ibada yao ya kishirikina na maadili ya ufisadi. Yeye mwenyewe alifuata dini ya Mtume Ibrahim, mtumishi wa kweli na Mwaminifu wa Mwenyezi Mungu. Hakumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote. Hakuwa mlevi na hakucheza kamari. Na alikuwa mwema kwa fukara na walioishiwa.
Mojawapo ya tabia za kutisha za Waarabu wakati ule ilikuwa ni kuwazika watoto wa kike wakiwa hai, punde wazaliwapo.
Pale ambapo Waraqa alisikia kwamba mtu alitaka kumzika mtoto akiwa hai, alikwenda kumshauri mtu huyo asifanye hivyo, na kama sababu ya kumuua mtoto huyo ilikuwa umaskini, alijitolea kumkomboa mtoto huyo na kumlea kama mtoto wake. Katika mifano mingi, baba wa mtoto alijutia kosa lake baadaye, na alikuja kumdai mtoto wake. Waraqa alikuwa akitaka ahadi thabiti kutoka kwa baba mhusika kumpenda mwanae wa kike na kumtendea wema, na hapo tu ndipo alipomruhusu amchukue.
Waraqa aliishi kwenye zama za ulimwengu wa upagani. Ulimwengu karibu ulikuwa unakaribia kufurika Mwanga wa Uislamu - Dini ya Mwenyezi Mungu - iliyo bora sana - Imani ya zama za kale, iliyoanzishwa karne nyingi za nyuma na Ibrahim Rafiki na Mtumishi wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Alikwisha mteuwa Mtumishi wake Muhammad Mustafa bin Abdullah, wa ukoo wa Bani Hashim, kuwa Mjumbe Wake mpya na wa mwisho hapa duniani. Mtume Muhammad (S.a.w.) alikuwa anaishi Makka wakati huo lakini alikuwa bado hajatangaza ujumbe wake.
Waraqa alikuwa mmojawapo wa watu wachache sana wa Makka walioelimika. Inasemekana alitafasiri Biblia kutoka kwenye lugha ya Kiebrania kuwa Kiarabu. Aidha alikwisha soma vitabu vingine vilivyoandikwa na wanatheolojia Wayahudi na Wakristo. Alikuwa mtafutaji makini wa ukweli ndani ya giza la dunia inayoendelea kuwa ndani ya giza nene zaidi, na alikuwa na nia ya kuupata ukweli huo kabla ya kifo chake, lakini hakujua angeupataje.
Khadija aliathiriwa sana na fikira za Waraqa na alikubaliana na Waraqa kuichukia ibada ya masanamu na watu waabuduo masanamu.
Hakumshirikisha Muumba na kitu chochote. Kama alivyokuwa Waraqa na ndugu wengine katika familia, naye pia alikuwa mfuasi wa Mitume Ibrahim na Ismaili.
Khadija alikuwa Muwahhid ( mwenye kumwamini Mungu Mmoja wa Pekee)! Khadija hakujua kwamba baada ya miaka michache hatima yake ingeingiliana na hatima ya Muhammad Mustafa, Mtume wa Imani ya Mungu Mmoja (Tauhiid); na hatima ya Uislamu, imani ya Mungu Mmoja.
Kabla ya Uislamu Bara Arabu ilikuwa haina mpango wowote wa kisiasa, na haikuwa na miundo mbinu ya aina yoyote. Hapakuwepo na mahakama au polisi au mfumo wowote wa sheria. Kwa hiyo, hapakuwepo na chombo cha kuzuia utendaji wa makosa, au kuwazuia wahalifu. kama Mwarabu alifanya kosa, hakuonyesha kujuta kokote. Badala yake alijivuna na kutamba kwamba angeweza kufanya lolote bila kujali, na kuweza kuwa katili na mkorofi.
Rasi yote ya Arabuni iliendeshwa kwa mfumo-dume. Mwanamke hakuwa na daraja kwa vyovyote vile. Waarabu wengi waliamini kwamba wanawake walileta mikosi. Kwa ujumla waliwaona wanawake kama mali inayohamishika na si watu.
Mwanaume aliweza kuoa wanawake wengi kwa idadi aliyopenda. Na wakati akifa, mtoto wake wa kiume wa kwanza aliwarithi wanawake (wakeze marehemu baba yake) wote isipokuwa mama yake. Kwa maneno mengine aliwaoa mama zake wa kambo wote isipokuwa mama yake aliyemzaa. Jambo kama hili, sheria na kanuni za maadili hazikuwepo kumzuia kwa njia yoyote ile. Uislamu ulisitisha desturi hii kisheria.
Waarabu walioishi kabla ya Uislamu hawakuwa na maadili mema. Mwarabu alitumia maisha yake yote kwenye ghasia za kivita. Mauaji na uporaji ilikuwa ndio kazi yake kubwa. Aliwatesa wafungwa wake wa kivita hadi kufa, na kuwatesa wanyama ilikuwa moja ya mambo yake ya kupitisha wakati. Mwarabu alikuwa na ukaidi wa hisia ya utukufu, ambao ulifanya auwe mtoto wake mwenyewe wa kike. Kama mkewe alizaa mtoto wa kike, alikuwa hawezi kuzuia uchungu na hasira zake.
"Na mmoja katika wao anapopewa khabari ya (kuzaliwa kwake) mtoto wa kike, husawijika uso wake ( huwa mweusi) akajaa sikitiko!.
(Akawa) anajificha na watu kwa sababu ya hatari mbaya aliyoambiwa! (anafanyashauri) Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni (karibuni na hali ya kuwa mzima ili afe)? Sikilizeni! Ni mbaya mno hukumu yao hiyo. (Quran 16:58-59)
Mara nyingi Mwarabu alimuua mwanae wa kike kwa kuogopa kwamba angekuwa mateka wa kivita wakati wa vita vya kikabila, na kwa hiyo, kuwa mtumwa wa adui, na daraja lake kama mtumwa kungeleta aibu kwa familia yake na kabila lake. Angeweza pia kumuua kwa kuhofia kwake umasikini. Aliamini kwamba binti yake angekuwa tatizo la kiuchumi kwake. Uislamu ulifanya mauaji ya watoto kuwa ni dhambi kubwa kabisa.
وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلَاقٍ ۖ نَحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُمْ ۚ إِنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْئًا كَبِيرًا {31}
"Wala msiwaue wana wenu kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni hatia kubwa." (Qur\'an 17:31).
Vilevile walikuwepo Waarabu ambao hawakuwaua watoto wao, lakini waliwanyang\'anya haki zao zote. Walifikiri kwamba kwa vile binti zao watakapoolewa watakwenda kuingia nyumba nyingine za waume wao, hapakuwepo na haja ya kutumia gharama yoyote juu yao.
Ilikuwa katika mazingira ya namna hii ambayo Khadija alizaliwa, akakua na kuishi mazingira ya "kumkataa mwanamke."
Kutokea nyumbani kwake Makka, Khadija aliendesha biashara iliyokuwa inaendelea kukua na kuenea kwenye nchi za jirani. Kile ambacho alikwisha faulu kukipata kingekuwa cha kusifika katika nchi yoyote, katika kipindi chochote na kwa mtu yoyote mwanamume au mwanamke. Lakini mafanikio yake yamesifika mara mbili pale ambapo mtu atafikiria ule "mfumo-dume" wa kumpinga mwanamke, ulioendekezwa na Waarabu. Huu ni uthibitisho wa uwezo wake wa kumudu hatima yake kwa kutumia akili yake, nguvu ya dhamira na tabia. Wafanyabiashara wenzake walikubali mafanikio yake walipomwita Malikia wa Makuraishi na Malkia wa Makka kama ambavyo imetamkwa huko nyuma.
Lakini zaidi ya sifa, Khadija pia alipata cheo cha tatu. Aliitwa "Tahira" maana yake ni "aliyetakasika." Nani aliyempa cheo cha "Tahira"? Ajabu ni kwamba, alipata cheo hiki, kutoka kwa Waarabu haohao waliokuwa na sifa mbaya kwa ujeuri, majivuno, kiburi na ujinsia. Lakini, tabia ya Khadija ilikuwa mfano mzuri wa kuigwa hivyo kwamba ilitambuliwa hata na wao, na wakamwita "aliyetakasika."
Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Arabuni kwa mwanamke kuitwa Malikia wa Makka na aidha kuitwa "Tahira." Waarabu walimwita Khadija Malkia wa Makka kwa sababu ya utajiri wake na walimwita Tahira kwa sababu ya utakatifu wa sifa zake. Pia walikuwa wanaelewa kwamba alikuwa na tabia njema. Kwa hiyo alikuwa mtu wa kuheshimika hata kabla ya Uislamu - kipindi cha Ujahiliya.
Ilikuwa ni jambo lisilopingika kwamba Khadija angetamaniwa na Waarabu mashuhuri na wana wa Wafalme. Wengi wao walipeleka posa ili wamuoe.
Lakini hakutaka kuolewa na yeyote kati yao. Wengi wa hao watu mashuhuri na wana wa Wafalme waling\'ang\'ania kutaka wamuoe.
Bila kukatishwa tamaa na kukataa kwake, waliendelea kutumia washenga wanaume na wanawake wenye kuheshimika kuendelea kumbembeleza. Lakini bado aliwakataa wote. Hii labda ni kwa sababu Khadija hakutilia maanani sana umuhimu wa uongozi wa mfumo-dume uliotawaliwa na wanaume katika jamii "inayowapiga vita wanawake."
Kukataa kwa Khadija kuolewa na Waarabu mashuhuri na wenye hadhi za juu, kulizua dhana nyingi kwamba ni mwanamume wa aina gani atakaye muoa. Lilikuwa ni Swali ambalo hata Khadija mwenyewe hakuweza kulijibu. Lakini majaliwa yalifahamu jibu lake; alikuwa aolewe na mwanaume ambaye si tu alikuwa bora kabisa kuliko wote katika nchi yote ya Arabu lakini alikuwa pia bora sana kuzidi viumbe wote. Ilikuwa ni majaliwa yake iliyomchochea kukataa maombi ya kuolewa na binadamu wa kawaida.