Bi-Zainab
WASIFU WA BI ZAINAB
Mmoja kati ya watu watukufu na wanaojulikana sana katika dini ya kislamu na haswa katika madhehebu ya Ahlulbayt a.s, ni siti huyu mtukufu Zainab bint Ali bin Abi Talib (Zainab al kubra). Hii ni kutokana na utekelezaji barabara wa majukumu makubwa na dhima nzito aliyotwisha. Ijapokuwa pana ugumu kuelezea historia yake kwa utendeti kwa kutomiliki maarifa kifu, tutakuwa ni wachoyo tusipomtaja lau kwa muhtasari.
Binti huyu jamali na jamili alizaliwa siku ya jumatano tarehe tano ya Mwezi wa Jamadul awwal mwaka wa tano baada ya hijra katika mji mtukufu wa Madina na kwa mara nyengine nyumba ya bw mtume s.a.w iligubikwa na bashasha. Kama Ilivyokuwa ada ya al- Imam Ali na mkewe bi Zahra a.s kutomtangulia bw Mtume s.a.w katika jambo lolote lile, hivyo hata jambo hili katiti la kumpa jina siti huyu walimuachia mbora wa viumbe.</p>
Waliokuwa walezi wakubwa wa Bi Zainab a.s msanjari na kaka zake ni bw Mtume s.a.w pamoja na mama yake bi Fatima na baba yake Imam Ali a.s. hivyo aliinukia kuwa ni binti shujaa, mwenye maadili kuntu na aliyepevuka kielimu na kifikira.
Bi Zainab a.s anajulikana kwa sifa nyingi zisizokuwa na kifani ila inayochipuka zaidi ni sifa yake ya kuwa mwanamke shujaa na mwanamapinduzi, Hii ni kutokana na mchango wake mkubwa na juhudi alizozifanya baada ya vita vya Karbala ili kufikisha ujumbe sahihi wa tukio hili la kuhuzunisha na pia kutengua uongo, porojo na propaganda nyingi zilizokuwa zimeenezwa na utawala dhalimu.
Miongoni mwa athari kubwa zilizopatikana kutokana na juhudi za Bi Zainab
1. Hakuna kipote cha kislamu kinachopinga uwepo wa matukio ya Karbala. (Utawala wa Yazid na Bani-Ummaya kwa ujumla walifanya juhudi kubwa ili kufuta tukio hili katika historia ya kislamu miongoni mwa vitu walivyofanya ni kubadilisha siku hii ya huzuni kuwa ni siku ya sherehe kupitia hadithi nyingi za kutungwa alizosingiziwa Bw. Mtume s.a.w. ila wasifue dafu kwani Bi Zainab aliasisi vikao vya kukumbuka siku na matokeo hayo)
2. Watu waliweza kuelewa uhalisi wa mambo .( mfano mzuri ni wakaazi wa mji wa Sham uliyokuwa makao makuu ya utawala wa bani Umaya, watu hawa walitakidi kuwa tukio la karbala lilikuwa baina ya watu waasi waliotoka kupinga uisilamu na utawala wa haki. Mantiki hii iliwapelekea kuwazomea watu wa nyumba ya mtume pindi walipoingizwa katika mji wa sham kama mateka wa kivita ila baada ya kusikia hotuba ya Bi Zainab a.s wengi waliangua kilio na kujutia vitendo vyao.)