Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
AQIDA

ujue ushia 01

2017/03/26

ujue ushia 01

 

Ni Nani Shi’a Ithna-shariyyah?

  Tunaeleza katika mwanzo wa utafiti huu nini makusudio ya neno Shi’ah, vipi limeanza, na kuenea kwa Ushi’a . Tunakuta katika kamusi za lugha kuwa neno Shi’a lina maana ya “Kufuata na wafuasi, na aghlabu limetumika jina hili kwa wafuasi wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na watoto wake mpaka likawa ni maalum kwao”.  

 Na wa mwanzo aliepanda mbegu ya Ushi’a katika Uislamu ni Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) naye ni wa kwanza kutamka jina la Shi’a kwa wafuasi wa Ahlul Bayt (a.s.) kama alivyopokea hayo As-Suyuti katika tafsiri yake Durrul-Manthur katika Ayah tukufu (Hao ni viumbe bora). Amesema: Amepokea Ibn Asakir katika Sanad yake kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillah amesema: Tulikuwa kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na akaingia Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) basi akasema Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.): “Naapa kwa ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake, hakika huyu na wafuasi wake wao ni wenye kufaulu siku ya Qiyamah na kwake imeteremka! “Hakika walioamini na kufanya vitendo vyema hao ndiyo viumbe bora.”1  

  Hivyo Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) alilingania Manhaj (njia) hii na akawafanyia Ahlul-Bayt (a.s.) wapenzi na wafuasi. Na utapata juu ya hayo katika sehemu ya kwanza ya utafiti huu, dalili zinazothibitisha wosia wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.)kwa Ahlul- Bayt (a.s.) wake kwa Uimamu katika ‘Ummah huu baada yake, kuanzia kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na kuishia kwa Al Imam Muhammad Mahdi Sahibu-z- Zamaan (a.s.) ambaye atadhihiri mwisho wa zama ili kujaza dunia kwa haki na uadilifu kama ilivyojaa dhuluma na ujeuri.      

Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) alipoaga dunia, kundi katika Masahaba, walionelea ukhalifa usiende kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), na Imam (a.s.) alikwishasema kwa kupinga kwake juu ya hilo kwa kukataa kwake kumbai Abubakr kwa kipindi cha miezi sita kama alivyopokea hayo Bukhari katika Sahih yake ambayo maelezo yake yatakuja katika sehemu ya kwanza kwa idhini ya Allah (s.w.t.). Na walikataa kumbai pamoja naye kundi la Masahaba wakubwa, mfano wa Zuber, ‘Ammar, Salman, Abudhar na wengineo. Kisha Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) alipoona kukataa kwake kunasababisha mbomoko usiotengenezeka katika Uislamu, na sote tunajua kuwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) hakuwa akitaka Ukhalifa wala hakutaka kutawala wala kupupia Ufalme na kushinda -   alikubali na akayafumbia macho yale anayo yaona kuwa ni haki yake kwa kuunusuru Uislamu kutokana na kubomoka na kuparaganyika. Wafuasi wake walibaki chini ya uongozi wake, na Ushi’a haukuwa na nafasi ya kudhihiri katika zama za Makhalifa wa kwanza, kwasababu Uislamu ulikuwa unapita katika manhaj yake iliyo sawa sawa.

    Na alipopewa Bai’a Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), Mu’awiyah bin Abi Sufian alikataa kumbai na akampiga vita katika sehemu ya Siffin, na alimtangulia kwa hilo ‘Aisha bint Abubakr as- Siddiq. Alitoka akiongoza jeshi linalompiga vita Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) katika vita vinavyojulikana kama vita vya Jamal. Masahaba wengi walijiunga pamoja na Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) katika vita vya Siffin hadi wengi wao wakauliwa chini ya uongozi wake, kama vile ‘Ammar bin Yaasir, Khuzaimatu Dhi Shahadatain, Abu Ayyubil-Ansari na wengineo.

  Na baada ya mambo kumnyookea Mu’awiyah bin Abi Sufian na kumalizika kwa duru ya Makhalifa, Mu’awiyah bin Abi Sufian alifuata sera ya madikteta, akawakandamiza Waislam na kuchukua Bai’a ya mwanae Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian kwa, ‘Ummah kwa mabavu, na akazikhalifu Ayah za Allah (s.w.t.) zilizo wazi, kama vile kumnasibisha Ubaydullah bin Ziyad kwa baba yake na kupanua meza za vyakula, kujenga mahekalu makubwa na mengineyo katika israf na upuuzi, yote hayo kwa mali za ‘‘Ummah na pato la Waislamu.  

  Haya yote na watu bado wako karibu na zama za Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na makhalifa, na namna walivyokuwa wakiyapanyongo mambo ya dunia na matamanio yake. Kisha akamtilia sumu Al Imam Hasan ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na akamuua baada ya kutengua ahadi na masharti yote aliyomuahidi, kisha akachukua bayi’a kwa mwanae Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian kwa mabavu na hali yake inajulikana kwa ‘Ummah bila ya kuwa na ikhtilafu - Waislamu walishamjua kuwa ni mtu wa dunia hana uhusiano na dini... mpaka yakatokea mapinduzi ya Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) Karbala, na kuuawa kwake Shahid pamoja na wafuasi wake wasiopungua sabini na mbili miongoni mwa Aali zake na wafuasi wake, baada ya kukataa kumbai Yazid bin Mu’awiyah bin Abi Sufian. Vivyo hivyo ulikuwa ni mwendo wa watawala wa Bani Ummayyah na Bani Abbas, katika kuwakandamiza Ahlul-Bayt (a.s.). Ukandamizaji kwa Ahlul Bayt (a.s.), ulikuwa kwa muda wote huo, na waliyapata (matatizo) mengi, miongoni mwayo ni kuuliwa, kufungwa jela na kuadhibiwa.    

Ukiuchunguza mwendo wa watoto wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) kwa ujumla, na ukaulinganisha na mwendo wa wafalme wa Bani Umayyah na Bani ‘Abbas, utagundua kuwa ndio umesababisha kuenea kwa Ushi’a ambao ndio Uislamu wa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na si vinginevyo, na wala si kama walivyosema wapumbavu ambao walikuwa wakikariri wanayo yaeneza watawala wa Bani Umayyah na Bani ‘Abbas kuwa Ushi’a ni upuuzi wa ‘Abdillah bin Saba’ au mengineyo yasiyokuwa hayo miongoni mwa uongo ambao unasambaratika mbele ya macho ya anayesoma Itikadi hata kwa uchache tu. Katika kipindi cha kwanza cha Bani Abbas, Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.) ambaye ni Imam wa Sita wa Mashi’a - kutokana na siasa yake ya hekima, aliweza kushirikiana na watawala na watu.

  Na kwa sababu ya watawala kushughulika na kuimarisha utawala wao - alianza kueneza hukumu na kusambaza Hadith ambazo alizichukua kwa baba yake Al Imam Muhammad Al-Baqir (a.s.) kutoka kwa baba yake Al Imam Zaynul ‘Abidiin (a.s.) kutoka kwa Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), Bwana wa Mashahid (na Imamu Hasan as), kutoka kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) kutoka kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.). Ushi’a ukadhihirika bila ya kuwa na mfano katika zama hizo, kupanuka Madrasah ya Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.) katika zama hizo na umashuhuri wake ndiyo sababu ya kuitwa madhehebu ya Ja’afariyyah katika manhaji (njia) ambayo Shi’a Imamiyyah Ithna- ’Ashariyyah wanaiamini tangu wakati huo hadi leo hii, na ambayo si kingine isipokuwa ni madhehebu ya Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.) na ambayo ndiyo dhehebu la ki- Islamu la asili.  

  Miongoni mwa waliokuwa wanafunzi wake wakubwa ni kama vile Hassan Al-Basriy na Abu Hanifa An-Nu’uman ambaye amesema katika kauli yake mashuhuri. “Kama sio miaka miwili angeangamia Nu’uman” alikuwa na maana ya miaka miwili ambayo alikuwa mwanafunzi katika darasa la Imam Jaafar bin Muhammad bin Ali bin Hussein bin Ali bin Abu Talib (a.s.) na ambaye amepewa laqab ya As-Sadiq. Abu Hanifa aliuawa kwa sumu katika jela ya Abu Ja’afar Al-Mansur kwa sababu ya mapenzi na ufuasi wake kwa Ahlul Bayt (a.s.), na kumpinga kwake Mansur, na kwa sababu alikataa cheo cha Qadhi katika utawala wake. (rejea chochote ukitakacho katika vitabu vya historia juu ya hilo) Mansur alimkataza kutoa Fatwa hali yuko ndani ya jela. Ama aliye eneza yanayojulikana kama madhehebu ya Hanafi ni Qadhi Abu Yusuf ambaye alikuwa mwanafunzi wa Abu Hanifa, Haruna Rashid alimpa uqadhi, jambo ambalo lilimsaidia katika kueneza madhehebu hayo. Ni maarufu katika tarikh kuwa madhehebu manne yamechipukia kwa Al Imam Ja’afar as- Sadiq (a.s.), Imam Malik amechukua elimu yake kutoka kwenye vitabu vya Abu Hanifa ambaye amesoma miaka miwili kwa Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.) kama tulivyo bainisha juu, kisha Shaf’i akachukua kutoka kwa Malik, kisha Imam Ahmad akasoma kwa Shaf’i. Hivyo kinacho patikana katika vitabu vya madhehebu manne na kikaafikiana na madhebu ya Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.), basi kimetoka kwa Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.); na kinacho tofautiana ni Ijtihad yao.    

Hakika Shi’a al-Imamiyyah Ithna-’Ashariyyah ni dhehebu ambalo limeepukana na Shub-ha na shaka, kwa sababu chini ya jina la Ushi’a yamechipuka makundi mengi sio katika Shi’a wala Shi’a sio miongoni mwa hayo na wala sio katika Uislamu hata chembe, Shi’a wako mbali nayo kama vile mbwa mwitu na damu ya Yusuf. Mfano wa baadhi ya madhehebu ambayo yamesema juu ya uungu wa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.), wakidai kuwa sehemu ya uungu ipo kwa Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib (a.s.) na imeungana na mwili wake, na baadhi yake yanasema kuwa Maimam ni Manabii wakidai kuwa wao ni waungu. Al Imam Ja’afar as-Sadiq (a.s.) alipojua Itikadi yao akawa mbali nao akawalaani na akawaambia wafuasi wake wawe mbali nao, na akatoa kauli kali juu ya hilo.

  Na sijui ni kwa nini tunaona baadhi wanAyahesabu makundi haya na mfano wake katika Ushi’a pamoja na kujulikana kwake kuwa yako nje ya Uislamu na Mashi’a wako mbali nayo.