Languages فارسی فارسى درى English اردو Azəri Bahasa Indonesia پښتو français ไทย Türkçe Hausa Kurdî Kiswahili Deutsche РУС Fulfulde Mandingue
Scroll down
Mafunzo-ya-kidini

Ziara ya Arbaeen

2016/11/17

Ziara ya Arbaeen

ZIARA YA AL IMAM HUSSEIN A.S

 

Taratibu ya kumzuru Imam Husayn (a) iliasisiwa na Watu wa Nyumba ya Mtume (s) waliohudhuria mauaji ya siku ya Ashura – yaani dada zake Sayyidna Husayn (a), Sayyidna Ali Zaynul-Abidin (a) na wengine… na baadae kutiliwa mkazo na maimamu wa Ahlul Bayt (a) mmoja baada ya mwingine.

Baada ya kuachiwa kutoka Sham, msafara wa Imamu ulirudi Karbala kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu. Walipofika kwenye uwanja wa vita wa Karbala, kila mwanamke alikwenda kwenye kaburi la wale wanaomhusu na kulia. Baada ya kuweka vikwazo vingi katika jela, wanawake walikuwa huru sasa kuwalilia mashahidi. Imamu Sajjad (a) alilia sana kwenye kaburi la mtukufu baba yake. Imamu wetu alikabiliana na mateso mabaya sana yasiyoelezeka; aliwaona wanawake wa nyumba yake wanafanyiwa unyama mbele ya macho yake, aliwaona watoto wa nyumba yake wanavyonyanyaswa, yeye mwenyewe aliadhibiwa vikali.

Sayyida Zainab (a) alilia sana kwenye kaburi la kaka yake aliyemshuhudia akichinjwa kama mbuzi. Alilia kwenye kaburi la kaka yake Sayyidna Abbas, maadamu alipokuwa hai, kwa ushujaa wake hakuweza mtu yeyote kuwanyang’anya hijabu zao. Baada ya muda wa siku tatu wa vilio na maombolezo, Imamu Sajjad (a) akamsogelea shangaziyake na akamjulisha ya kwamba wakati umewadia wa kujitayarisha kuondoka kwenda nyumbani. Karbala walikuja wakiwa na ndugu na jamaa, makaka na watoto, leo wanarudi nyumbani wakibeba mzigo wa majonzi na vilio. Bila kutaka, msafara uliaga makaburi ya mashahidi na ukaanza safari yake kuelekea Madina.

Njia nzima, popote msafara uliposimama, Sayyida Zainab (a) aliongoza majlis ya kumkumbuka Imamu Husayn (a) alivyojitoa muhanga kule Karbala. Aliwafikishia watu usia wa mwisho wa Imamu (a) kwa wafuasi wake, ujumbe wake wa kutenda mema na kukataza maovu, ujasiri wake dhidi ya khalifa jeuri na fedhuli na urithi wake wa kutoa muhanga kila kitu ulichonacho ili KUNUSURU ujumbe wa kweli wa Uislamu. Imethibiti katika historia kwamba Imam Ali Zaynul-Abidin (a) alikuwa akifanya ziara ya kaburi la baba yake na mashahidi wengine huko Karbala.Zimepokelewa hadithi nyingi kutoka kwa Maimamu wa Ahlul Bayt (a), zinazotilia mkazo kumzuru Sayyidna Husayn (a) na kwamba ni amali yenye thawabu nyingi. Maimamu waliandika ziyarah za kusoma pindi tunapozuru.Moja wapo ya ziarah ni Ziyaratul Waritha.

 Hapa tunataja riwaya chache za maimamu zinazosisitiza jambo hili :

-Imam Ali bin Husayn (a) alisema:

“waamrishe Mashia wetu kufanya ziara ya kaburi la Husayn bin Ali (a). Huu ni wajib wa kila mUislamu ambae anakubali uimamu wa Husayn (a)”.

-Imam Ja’far Sadiq (a) alisema:

“Yeyote atakayefurahia kuwepo kwenye meza za nuru Siku ya Qiyama, basi afanye awepo miongoni mwa wale wanaofanya ziara ya Husayn bin Ali”.

 

-Imam Musa al-Kadhim (a):

“Thawabu ya chini kabisa atakayopewa yule anayemzuru Husayn (a) ukingoni mwa mto Furati, ni kusamehewa madhambi yake yaliyotangulia na ya baadae, ikiwa anatambua haki yake, utakasifu wake na mamlaka yake kama Imam.”

Ziara ya makaburi :- yaani kuwazuru mitume, mawalliy na waja wema wa Allah, ukawaombea, ukasali na kutabarruku kwa Baraka zao ndiyo hasa kusimamisha Tawhid. Jambo hilo limethibiti katika Qur’ani, sunna sahihi ya Mtume (s), Maimamu wa Ahlul Bayt (a), na ulamaa.

 Pia limethibiti kiakili na mwenendo wa masahaba na matabiina. Katika Sunan, Ibn Maja, anasimulia kwamba Mtume (s) aliamrisha:

“Zuruni makaburi kwani hilo litawakumbusha Akhera”.

                                                                                                                         (vol. L, 235)

Muslim, Ibn Maja na Nisa-i, wote wanaripoti kwamba Abu Hurayrah alisema:

“Mtume alizuru kaburi la mama yake. Akalia na kuwafanya waliomzunguka kulia.”

Ni ajabu mawahhabi leo kutegemea maoni ya mtu mmoja ambaye ni Ibn Taymiyyah (661-728) ambaye alisema kuzuru kaburi la Mtume (s) ni haramu, sembuse makaburi mengine. Leo Mawahhabi wanawakufurisha Waislamu kwa ujumla kwa maoni ya mwanazuoni mmoja kwa kutegemea hoja dhaifu! Ikiwa shirk twaielewa, basi hii ni shirk ya kuwachukua ulamaa wetu kuwa ni ‘arbaab’ (9:31)

Shamsuddin, Muhammad Mahdi:The Rising of Al Husayn: its impact on the Consciousness of Muslim Society, p. 35