Upeo wa ufasaha
Khutba Ya Kwanza
Anayestahiki sifa njema ni Allah (s.w.t) ambaye ubora wa sifa zake hawa ufikii wasemaji. Ambaye neema zake wahasibu hawawezi kuzihisabu. Wenye juhudi hawawezi kutekeleza haki ya utii wake. Ambaye fahamu ya hali ya juu ya wenye akili haiwezi kumfikia kumtambua,1 wala, utambuzi wa kina hauwezi kumuelewa 2 ambaye sifa zake hazina mpaka wenye kikomo,3 wala hana sifa. Wala wakati uhisabiwao, wala muda uliowekwa.4 Ameumba viumbe kwa uwezo wake, na ameutawanya upepo kwa rehema zake; kwa milima ameimarisha uyumbaji wa ardhi yake. La kwanza katika dini ni kumtambua yeye,5 na ukamilifu wa kumtambua ni kumsadiki, na ukamilifu wa kumsadiki ni kumpwekesha.6 Na ukamilifu wa kumpwekesha ni kumtakasa na ukamilifu wa kumtakasa ni kumuepusha mbali na sifa. Na mwenye kumsifu Mwenyezi Mungu swt. Atakuwa amemuambatanisha,7 na mwenye kumuambatanisha amemfanya kuwa wawili,8 na mwenye kumfanya kuwa wawili atakuwa amemfanya kuwa mwenye sehemu sehemu, na mwenye kumfanya kuwa mwenye sehemu sehemu atakuwa hamjui (s.w.t.), na asiyemjua atakuwa amemuonyesha, na mwenye kumuonyesha atakuwa amemwekea mipaka,9 na mwenye kumuwekea mipaka atakuwa amemuhisabu.10 Na mwenye kusema yuko ndani ya nini? Anakuwa amemwingiza (s.w.t) ndani ya kitu.11 Na mwenye kusema yuko juu ya nini? Atakuwa amemtoa humo.12 Amekuwa yupo sio kwa kutukia, yupo lakini sio kwa maana ya hakuwapo hapo kabla. Yuko pamoja na kila kitu si kwa mwambatano wa kimwili.13 Yutafauti na kila kitu si utafauti wa kimwili, mtendaji sio kwa maana ya harakati za kimwili na vyombo, mwenye kuona pindi hakuna wakuonwa kati ya viumbe wake. Yu pweke pindi hakuna mkazi analiwazika naye wala haoni ukiwa kwa kukosekana kwake. A. Kuumbwa Kwa Ulimwengu. Alianza kuumba viumbe mwanzo, na kuvibuni kwa ubunifu, bila ya kupitisha fikra, wala kufaidika na uzoefu wowote, wala hakufanya harakati yeyote, wala kusumbuliwa na azma ya ndani ya nafsi, amevitoa viumbe (kutoka hakuna kitu na kuviingiza) kwenye ulimwengu wa kuwepo kwa wakati wake. Akaviunganisha viumbe pamoja na tofauti zao. Akaweka silika zao, na akaziambatanisha hizo silika na wenyewe. Akiwa mjuzi (s.w.t) kabla hajabuni (viumbe) akiwa mwenye kuelewa kwa ukamilifu, mipaka yao na mwisho wao, akiwa mwenye kutambua utashi wao na sehemu zao nyingi. Kisha aliumba (s.w.t.) mwanya wa anga na eneo la mbingu na utando wa upepo, alimimina humo maji ambayo mawimbi yake yalikuwa makali na mawimbi yalilundikana moja juu ya jingine, aliyabebesha kwenye upepo uendao kwa kasi, na mtikisiko mkali, na kimbunga kinachovunja. Aliyaamrisha yamwage (mvua) aliufanya upepo uwe na uwezo wa kuzuia nguvu za mvua na kuijulisha mipaka yake. Upepo ulivuma chini hali maji yalibubujika kwa kasi kwa upande wa juu. Kisha (s.w.t.) aliumba upepo ambao ulifanya mvumo wake uwe tasa. Yaani mvumo wa hewa ulifanywa usioweza kurutubisha kizazi, kwa kuwa kuna upepo urutubishao mimea na kuifanya itoe mazao. Na upepo huu uli- umbwa ili kuyatikisa maji tu. Na akadumisha kubaki kwake, mwendo wake ulishika kasi na akayatawanya kwa umbali na kwa upana. Kisha aliuamrisha upepo kuyanyanyua maji yalio kwenye kina, na kuongeza kasi ya mawimbi ya bahari. Yakatikisa mtikiso kama ule ufanywao kwa kinywaji cha maziwa. Na kuvuma nayo angani. (Anakusudia kueleza kuwa upepo ukivuma angani anga ambazo ziko tupu huwa mvumo wake mkali kwa sababu ya kutozuilika na kitu chochote, na upepo huu ulivuma na maji mengi mvumo mkali sana). Wayarudisha ya mwanzo nyuma na yaliyotulia kuyapeleka kwa yaliyo kwenye mtikisiko, mpaka yakainuka mwinuko. Na sehemu ya chini ilijaa povu. Baadaye Mungu (s.w.t.) aliinua povu lile juu ya upepo ulio wazi kutoka humo aliumba mbingu Saba. Na sehemu ya mawimbi ya chini aliyazuia na kuwa kituo, na ya juu kuwa kama dari inayo zuia na jumba lililoinuka bila ya nguzo zenye kulikinga, wala misumari inayo imarisha, kisha alizipamba (mbingu) kwamapambo ya nyota na mianga yenye nuru. Na alipitisha humo jua lenye taa yenye kuenea mwanga wake. Na mwezi wenye nuru katika sayari zinazozunguka. ,